Mhadhiri UDSM achaguliwa kuwania ubunge EALA

Dodoma. Kamati ya wabunge wa CCM imemchagua Gladnes Salema kukiwakisha chama hicho katika uchaguzi wa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) utakaofanyika Septemba 5, 2024 bungeni.

Dk Gladnes, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amewashinda wapinzani wake wawili ambao ni Lucia Pande na Queenelizabeth Makune.

Uchaguzi huo uliofanyika leo Jumatatu Septemba 2, 2024 katika ukumbi wa NEC White House, unalenga kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk Shingo Sedoyoka aliyefariki dunia Juni 13, 2024.

Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi huo, Issa Haji Gavi alitangaza wabunge watapigia kura majina tisa kwa awamu ya kwanza, ili kupata washindi wa watatu.

Baada ya washindi hao watatu kupatikana, walipigiwa kura tena ili kupata na mshindi mmoja atakayekwenda kupigiwa kura na wabunge wote wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano Tanzania.

Katika awamu ya kwanza ya uchaguzi huo, Dk Salema aliongoza kwa kupata kura 61, akifutiwa na Lucia Pande (49), QueenElizabeth Makune (44).

Wengine na kura zao katika mabano ni Fatma Kange (42), Theresia Dominic (32), Profesa Neema Kumburu (15), Fatma Msofe (7), Hawa Nkwera (5) na Maria Sebastian (4).

Baada ya matokeo hayo katika uchaguzi ulikuwa wazi, Gavi alitangaza washindi watatu wanaoingia katika awamu ya pili ya uchaguzi kuwa ni pamoja na Lucia, Dk Gladnes na QueeneElizabeth.

Akizungumza baada ya kura kuhesabiwa, Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Kassim Majaliwa aliwataka wabunge hao kurejea tena katika ukumbi huo baada ya kuahirishwa kwa Bunge.

“Baada ya msimamizi kutangaza matokeo haya ya awali, tutalazimika kwenda bungeni tukapitishe muswada. Kwa sababu kwa kanuni za Bunge kwa idadi yao hawataweza kupitisha muswada. Kwa hiyo inabidi twende bungeni kupitisha muswada, Katibu Mkuu wa CCM anatuhitaji tena hapa,”amesema.

Amesema watakaporejea ambapo wagombea wote tisa watapata nafasi ya kushukuru na kupata neno la chama.

Naye Gavi amesema kwa awamu ya kwanza kabla ya baadhi ya wabunge kurudi bungeni walipiga kura wabunge 269, lakini awamu ya pili walipiga kura wabunge 244.

Aidha katika uchaguzi huo kila mgombea alipewa nafasi ya dakika tatu kujielezea kwa wabunge na kisha kuulizwa maswali kwa lugha ya Kingereza.

Juzi, Kamati Kuu ya CCM iliteua makada wake 10 kugombea ubunge wa EALA, ili kujaza nafasi moja iliyoachwa wazi na Dk Sedoyokaa.

Uamuzi wa kamati kuu hiyo uliwakata makada wengine 37 waliotia nia kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kuwania ubunge wa EALA.

Related Posts