Dodoma. Mashahidi 10 wameshatoa ushahidi wao kwenye kesi ya jinai inayowakabili washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile, binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Mpaka Agosti 30, 2024 jumla ya mashahidi sita walikuwa wameshatoa ushahidi, akiwemo binti anayedaiwa kufanyiwa vitendo hivyo aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la XY
Leo Jumatatu September 2, 2024 jumla mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri wametoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule na kufanya jumla ya mashahidi waliotoa ushahidi wao kufikia 10.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, wakili anayewawakilisha washtakiwa hao, Meshack Ngamando amesema mwenendo wa kesi hiyo ni mzuri, kwani mawakili wa utetezi wamepata muda wa kuwasikiliza na kuwahoji mashahidi walioletwa na upande wa Jamhuri.
“Kesi hiyo itaendelea kesho panapo majaliwa ya uzima na upande wa Serikali utaendelea kuleta mashahidi…. Kesi hii itaendelea kusikilizwa mfululizo mpaka upande wa Jamhuri utakapomaliza kuwaleta mashahidi wao na kama washtakiwa watakuwa na kesi ya kujibu na sisi tutaleta utetezi wetu mahakamani,” amesema Ngamando.