Simulizi ya msichana aliyesafiri kwa pikipiki nchi tisa Afrika

Dar es Salaam. Miezi takribani mitatu ilimtosha Ebaide Udoh (27), kukamilisha safari ya peke yake aliyoifanya kwa kutumia pikipiki kufika nchini Nigeria akitokea Kenya.

Akiwa anaishi Kenya tangu mwaka 2022, aliamua kufanya safari hiyo kama sehemu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwenda katika ardhi ambayo alizaliwa na kuishi.

Woga uliochanganyika na furaha ya kufanya safari hiyo, ni vitu vilivyokuwa vikimsonga muda wote, hasa alipolazimika kuendesha katikati ya pori bila kukutana na gari, pikipiki wala mtu.

“Kuna sehemu nilikaa peke yangu porini kwa muda mrefu nisione mtu, gari wala pikipiki. Hali hii ilinifanya kushangilia nilipoona kijiji au sehemu ambayo watu wapo, ile hali ya woga ilikuwa ikiondoka moyoni mwangu,” amesema Ebaide alipozungumza na Mwananchi kupitia mtandao wa WhatsApp.

Akiwa ni mwanamke wa kwanza kuendesha pikipiki kutoka Afrika ya Mashariki hadi Afrika ya Magharibi, hadi kufika Nigeria, alilazimika kupita katika nchi za Uganda, Rwanda, Tanzania, Zambia, Angola, Jamhuri ya Congo na Cameroon.

Akitumia zaidi ya kilomita 11,000 barabarani, kuna wakati alilazimika kupata usaidizi au mtu wa kumsindikiza hasa alipokuwa akikatisha sehemu hatarishi kama hifadhi za wanyama, ikiwemo Katavi iliyopo Mkoa wa Katavi, nchini  Tanzania.

“Kuna sehemu nilishauriwa na wenyeji kuwa nipate mtu wa kunisindikiza, nilifanya hivyo, huko tulikutana na wanyama wakali, akiwemo tembo na nilijiuliza ningekuwa mwenyewe ingekuwaje,” amesema.

Ebaide ambaye alitunza kumbukumbu ya safari yake yote kwa njia ya picha mjongeo (video), pia alikuwa akichapisha vipande vya safari ya siku husika kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram, jambo lililofanya watu wengi kujua kinachoendelea katika safari yake.

Katika safari hiyo, alilazimika kubeba gorodo na mto wa upepo, hema, jiko dogo la gesi, birika kwa ajili ya kuchemshia kahawa, begi dogo la plastiki kwa ajili ya kuweka maji likiwa na uwezo wa kubeba lita 20.

Kwa mujibu wake, maji aliyokuwa akiweka katika begi hilo ndiyo pia alikuwa anatumia kuoga, kwani wakati mwingine alilazimika kulitundika juu ya mti ili aoge.

Mbali na vitu hivyo, pia alikuwa na makoti mawili moja likiwa la mvua, suruali mbili, kaptura mbili na shati tatu (crop top).

Ebaide amesema awali lengo lake lilikuwa  kuendesha pikipi kutoka Kenya hadi Uganda, lakini baadaye aliamua kuongeza safari hadi kufika nchini Nigeria, ikiwa ni sehemu ya yeye kufanya kile anachokipenda (kuendesha pikipiki) na utalii ndani yake.

Licha ya kuwa dereva wa pikipiki, hii ni safari yake ya kwanza ndefu kuwahi kuifanya ambayo imekatisha katika nchi kadhaa, kwani mwaka 2016 aliwahi kwenda Ghana jambo ambalo lilianza kujenga matamanio ya yeye kusafiri umbali mrefu zaidi, hasa aliponunua pikipiki yake.

Baadaye Machi 2024 ndiyo alianza safari ya ndoto zake na hatimaye Juni 30, 2024 alifika Nigeria.

Pamoja kiu ya kufanikisha kile alichokuwa amepanga, wakati mwingine alikutana na changamoto ambazo zilimuogopesha hasa alipokuwa akijikuta hatarini muda wote kutokana na waendesha pikipiki kudharauliwa wanapokuwa barabarani.

Hiyo ni kutokana na watumiaji wengine wa barabara hasa wanaoendesha magari, madereva wa malori kujiona kuwa na uwezo wa kuepuka chochote na kwa haraka zaidi.

“Sidhani kama wanawaona binadamu kwenye pikipiki. Nafikiri wanaona tu mashine. Wanaweza kukusukuma barabarani na gari lao, ili tu uendelee kukaa pembeni mwa barabara. Na ukweli ni kwamba pembeni mwa barabara ni sehemu hatari zaidi kukaa,” amesema Ebaide.

Amesema waendeshaji wa pikipiki za biashara zinatofautiana na waendesha pikipiki binafsi, hivyo ni vyema Serikali za nchi tofauti zikaona umuhimu wa kuweka sheria bora za kuwalinda waendesha pikipiki.

Pia ubovu wa barabara ni changamoto nyingine amekutana nayo katika maeneo tofauti, jambo ambalo linaongeza hatari kwao.

“Kuna kazi kubwa ya kufanywa katika nchi tofauti, kwani barabara bora zitasaidia kwa usalama, usalama wa maisha na mambo mengine mengi, ikiwemo kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Ebaide.

Upatikanaji wa viza kwa ajili ya kutoka nchi moja kwenda nyingine nayo ni changamoto aliyokutana nayo iliyomlazimu kutumia siku kadhaa au kutumia hela zaidi ya kiwango kinachohitajika, ili apate viza kwa siku chache.

Wakati mwingine ugumu wa kupata viza ulimfanya kubadilisha njia aliyokuwa amepanga kuitumia kukwepa usumbufu na kuamua kupita nchi nyingine.

“Maisha yangu yangekuwa rahisi zaidi kama ningeingia Angola kupitia Namibia, yaani Zambia, Namibia, Angola. Lakini nilijaribu kupata visa ya Namibia sikufanikiwa na tayari nilikuwa nimetumia pesa nyingi kwenye visa. Kwa hivyo ilibidi nipite DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo),” amesema Ebaide.

Jambo hilo lilimfanya kutumia fedha nyingi hasa linapokuja suala la usalama, jambo lililomfanya aisafirishe pikipiki yake kutoka Soyo nchini Angola hadi Pointe-Noire sehemu ya Jamhuri ya Kongo.

Kwa mujibu wa Ebaide, ipo programu mtandaoni zinazomuwezesha mtu kujua sehemu yoyote anayotaka kwenda na gharama anazoweza kutumia tofauti na Google map ambayo imezoeleka.

Kupitia prgramu hiyo, pia huweza kujua hata hoteli zilizopo na vitu vingine.

 “Hii ni rafiki kwa wasafiri. Waendesha pikipiki wengi hutumia programu hiyo. Kwa hivyo wanakueleza mara nyingi, mahali pa kuegesha pikipiki yako unapofika, mahali pa kula, bei na kituo cha mafuta kilicho karibu zaidi. Ni programu nzuri, programu ya Overlander nayo imenisaidia sana,” amesema.

Amesema uwepo wa programu hiyo ilimsaidia sana, kwani wakati mwingine kabla hajaanza kwenda mahali fulani alikuwa akipiga simu na kama lugha inayotumika anaielewa alikuwa huru kuuliza maswali.

“Kuna mengi mtandaoni kutoka kwa watu ambao tayari wamefanya hivi kabla, kwa hivyo sikuwahi kusafiri bila taarifa. Ilikuwa rahisi kidogo,” amesema.

Wakati mwingine amesema alikuwa akipata hoteli ambazo alijua hawezi kukaa usiku mzima, lakini pia yalikuwapo maeneo mazuri.

Moja ya sehemu aliyolala anaikumbuka ni Liazumbi njia ya kwenda Sumbawanga mkoani Rukwa au Katavi ambapo chumba alichopata hakikuwa kinamuwezesha kufunga mlango na kulala kwa uhuru.

“Hali ile ilinifanya nisogeze kitanda hadi mlangoni, angalau nizuie mlango kwa kutumia kitanda kwa sababu nilikuwa ugenini,” amesema Ebaide.

Jamii ilimchukuliaje barabarani

Kuwa mwanamke anayeendesha pikipiki kutoka sehemu moja kwenda nyingine, anakiri kutokutana na changamoto au mitazamo hasi kutoka kwa watu na badala yake watu walipomuona walimchangamkia na kumpokea kwa furaha.

Amesema kila watu walipomuona walivutiwa zaidi na kutaka kumjua kwa undani zaidi.

Abaide anasema ikiwa unataka kufanya jambo lolote usijali watu wanasema nini, bali nafsi ya mtu ni lazima ihakikishe umedhamiria unachotaka kufanya na kuwekea nguvu.

“Watu watasema mambo mengi na mara zote ukitaka kupiga hatua kubwa lazima utaogopa. Sasa hapa watu huwa wanaogopa kisichojulikana na mara zote watajaribu kukosoa kila wakati, hasa wanaposhindwa kuelewa,” anasema Abaide.

Baada ya kumaliza kwa safari yake ya awali, sasa anapanga kufanya safari nyingine kati ya Nigeria hadi Moroco kuanzia Septemba 28, 2024 ambayo anatarajia kupita katika nchi 15.

“Lengo langu ni kuzunguka kuendesha pikipiki katika nchi zote 54 za Afrika, nimalize Bara la Afrika,” amesema Ebaide.

Related Posts