Madiwani Simanjiro walia fidia ndogo inayotolewa na Tawa

Simanjiro. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamelalamikia fidia kidogo wanayopata kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (Tawa), wanapopata  majanga mbalimbali yanayosababishwa na wanyamapori.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Septemba 2, 2024 na madiwani hao katika kikao cha Baraza la Madiwani.

Alikuwa ni Diwani wa Naisinyai, Taiko Kurian Laizer ambaye amesema baadhi ya wananchi wa eneo lake walijeruhiwa na tembo ila hawakulipwa  na Tawa japokuwa walitoa taarifa.

“Zaidi ya hayo, hata hiyo fidia inayosemwa itatolewa pindi mtu akipata majanga ni ndogo, kwa sababu wanyamapori wakishambulia mtu au wakila mazao fidia inayotolewa ni kidogo mno,” amesema Taiko.

Hata hivyo, mkuu wa Tawa idara ya ujirani mwema ikolojia ya Handeni Kitwai, Ambokile Mwakyusa amesema kumepitishwa sheria mpya na kanuni zake za fidia pindi wanyamapori wakijeruhi, kuua au kuharibu mazao.

Mwakyusa amesema viwango hivyo vimebadilika na mtu akiuawa na mnyama kinatolewa kifuta machozi cha Sh2 milioni, awali ilikuwa Sh1 milioni na mtu akijeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu alikuwa anapata Sh500,000 na sasa ni Sh1 milioni na kama ni ulemavu wa kupona anapata Sh500,000.

Amesema kwa upande wa mazao wanatoa fidia kwa ekari moja Sh375,000 pindi wanyamapori wakifanya uharibifu.

Diwani wa Msitu wa Tembo, Kaleiya Mollel amesema matukio ya mazao kuliwa na tembo au watu kujeruhiwa yametokea mara nyingi ila hawapati fidia wala kifuta machozi.

Naye Diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi amesema jamii inalalamikia changamoto hizo hivyo Tawa wachukue hatua kwa kurekebisha viwango vyao.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jacob Kimeso amesema kuna baadhi ya wanyama wanaua watu ila hawapo kwenye orodha ya fidia, hilo linapaswa kuangaliwa.

“Kwenye orodha ya Tawa hakuna majina ya nyoka au kicheche katika  kulipwa fidia na watu wengi wanaathirika mno kutokana na wanyama hao, hili litazamwe upya, kwa sababu wapo nyoka wakubwa kama chatu na wengineo, madhara yake ni makubwa pale wanapomgonga mtu,” amesema Kimeso.

Amesema kwenye kata yake ya Edonyongijape kuna watu wawili walifariki dunia kwa kung’atwa na mnyama kicheche ambaye ana sumu na hakuna fidia yoyote waliyopata kutoka Tawa.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Baraka Kanunga amemuagiza kiongozi huyo wa Tawa kufikisha kwenye mamlaka yake yale yote yaliyolalamikiwa na madiwani, ili yafanyiwe kazi.

“Nadhani umewasikiliza vyema waheshimiwa madiwani walivyosema hoja na changamoto zao, hivyo fikisha kwa viongozi wako ili waweze kutekeleza hayo,” amesema Kanunga.

Related Posts