Maeneo tofauti nchini Tanzania yanashuhudia mvua kubwa ambazo sio tu zinaathiri miundombinu na kuhatarisha usalama wa maisha ya watu bali pia inaweza kuwa hata kwa vifaa vya umeme nyumbani.
Watu wengi huingia hasara wakati vyombo vyao vya umeme walivyovinunua kwa gharama kubwa kuharibika kutokana na hitilafu za umeme. Mara nyingi matukio ya aina haya yanaweza kuzuilika endapo tahadhari zikichukuliwa mapema.
Akizungumzia kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia, Meneja wa Bidhaa za Kieletroniki wa Samsung Tanzania, Bw. Evans Songa ametolea ufafanuzi maswali ya msingi ambayo wateja wengi wamekuwa nayo hususani kwa wanaoishi na familia au wenyewe, ili kuhakikisha usalama wa vyombo vya umeme nyumbani.
Swali: Kuna hatari zipi za kushika vyombo vya umeme kwa mikono ikiwa na maji?
Jibu: Bila shaka wote tunafahamu kwamba maji na umeme haviendani. Madhara ya kutumia vyombo vya umeme mikono ikiwa imelowana ni pamoja na mtumiaji kupigwa shoti ya umeme. Pia, unaweza kusababisha shoti kwenye kifaa chako. Kuna baadhi ya vifaa vinakuelekeza uhakikishe kuwa ni vikavu kabla ya kuchomeka katika soketi ya umeme.
Swali: Nini kinashauriwa baada ya kumaliza matumizi ya vyombo vya umeme nyumbani?
Jibu: Kuna baadhi ya watu wana kawaida ya kuacha vyombo vyao katika soketi za umeme baada ya kumaliza matumizi. Mbaya zaidi wengine husahau hata kuzima kabisa kutokana na vifaa vingi vya siku hizi ni automatic hivyo kujizima vyenyewe mara tu vikimaliza kazi iliyokusudiwa. Tabia hii inaongeza hatari ya chombo kuharibika au kuungua endapo kutatokea shoti ya umeme.
Swali: Kuna faida gani ya kusafisha vyombo vya umeme mara kwa mara baada ya kumaliza matumizi?
Jibu: Inashauriwa kusafisha vyombo vyako vya umeme mara tu baada ya kumaliza matumizi. Hii itakusaidia kulinda vyombo vyako hususani kwa kuvieupusha na mazingira ambayo yanaweza kuleta kutu. Ukiachana na kusafisha pia hakikisha unakuwa unavitumia vyombo vyako mara kwa mara ili kujua kama vinafanya kazi kwa ufasaha au la. Sidhani kama utafurahi siku ambayo una uhitaji zaidi wa chombo chako na kugundua kuwa hakifanyi kazi aidha kutokana na kutokitunza au kujaribu kama kinafanya kazi mara kwa mara.
Swali: Kuna umuhimu gani wa kuwa na warantii kwa vyombo vya umeme?
Jibu: Kwanza kabisa, kwa wasiofahamu warantii ni dhamana ya muda maalumu inayotolewa kwa ajili ya matazamio ya bidhaa ili kumhakikishia mtumiaji juu ya ubora na ufanyaji kazi wa bidhaa husika. Sio kampuni zote zinatoa warantii kwa bidhaa wanazouza kwa wateja wake. Lakini kuna makampuni ambayo yanazingatia hili ili kuwaridhisha na kuwapatia amani wateja wake dhidi ya hofu ya vyombo vyao pindi vikipata hitilafu.
Ukiachana na warantii, pia humhakikishia mteja kupata huduma kutoka kwa wataalamu wao wenye weledi, huduma kwa mteja ya uhakika, vifaa halisi marekebisho yakihitajika, pamoja na kupokea taarifa za mara kwa mara kuhusu kifaa husika. Kigezo muhimu cha kupata warantii ni kununua bidhaa kutoka kwa mawakala wa bidhaa waliohakikiwa pamoja na kuwa na kadi ya warantii kwa bidhaa za nyumbani.
Kwa kumalizia, familia nyingi zinatumia vyombo vya umeme nyumbani kutokana na maendeleo ya kiuchumi yanayochochewa na uvumbuzi katika sekta ya sayansi na kiteknolojia. Kuongezeka kwa makampuni ya utengenezaji na usambazaji wa vifaa hivyo pia kumepelekea urahisi na unafuu wa upatikanaji wake.