Kichanga chafariki baada ya kudaiwa kubakwa na baba yake

Dodoma. Mkazi wa Mtaa wa Mbuyuni, katika kata ya Kizota mkoani Dodoma, Stephen Damas (38) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti hadi kusababisha kifo cha mtoto wake mwenye umri wa miezi sita.

Tukio hilo lilitokea eneo la Mbuyuni, kata ya Kizota jijini Dodoma jana Septemba mosi, 2024 saa 3.00 usiku na kisha kutelekezwa mwili wa mtoto huyo wa kike nyumbani kwa bibi yake.

Akizungumza leo Jumatatu, Septemba 2,2024, Bibi wa marehemu, Elizabeth Sudai amesema jana saa 3.00 usiku alikuja mkwe wake (Stephen) na kumgongea mlango.

“Nilikuwa nimelala, akaniita, mama, mama mjukuu wako huyo hapo. Mimi nikatoka, nikakuta mtoto amelazwa kizingitini. Niangalie aliyemleta mtoto, nikaangaza lakini sikumpata,”amesema.

Amesema alivyombeba mtoto aliona hatikisiki na amelegea, hali iliyomfanya kutafuta majirani zake na walipofika aliwaeleza kilichotokea.

Amesema walishauriana  kwenda kwa balozi na kisha hospitali ambapo iligundulika mtoto huyo amefariki dunia, baada ya kubakwa na kulawitiwa.

Balozi wa Shina namba tano, katika Mtaa wa Mbuyuni,  Tausi Rashid amesema baada ya mtoto huyo kufikishwa kwake na alipomuangalia aligundua hatikisiki na hana fahamu.

Amesema hali hiyo ilimfanya kumpigia simu polisi kata ambaye alitoa maelekezo waende kituo cha kati cha polisi.

Amesema walikwenda polisi na baadaye hospitali ambapo walibaini kuwa mtoto huyo alilawitiwa.

“Nikamuuliza mama yake kama walikuwa na ugomvi, akasema hawakuwa na ugomvi wowote siku ya jana na kwamba baba alimchukua mtoto akawa anacheza naye ndani,”amesema.

Amesema baada ya hapo ilipofika saa 1.00 jioni jana, baba huyo alitoka na mtoto kama anaelekea dukani na hivyo hakuwa na hofu yoyote.

Hata hivyo, amesema ilipofika saa 2.00 usiku, alimtafuta mumewe bila mafanikio hadi muda huo alipomtafuta na kukuta tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma George Katabazi amesema mtuhumiwa ambaye ni baba mzazi wa mtoto amekamatwa na  wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

“Mtuhumiwa tumeshamkamata, tunaendelea na taratibu nyingine za kiuchunguzi. Jamii iendelee kushirikiana na jeshi la Polisi kwa kuwa masuala haya ya ukatili wa kijinsia na watoto ni mtambuka, ili kukomesha ukatili huu,”amesema.

Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi kujua sababu za mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo.

Related Posts