Dodoma. Serikali imesema mwaka wa fedha 2024/25, itajenga jumla ya nyumba za walimu 562 zinazotosha familia 1,124.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 30, 2024 na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainabu Katimba wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Jacqueline Andrew.
Andrew amehoji mpango wa Serikali katika kujenga nyumba za walimu nchini.
Akijibu swali hilo Katimba amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari nchini inayotakiwa kutatuliwa.
Katimba amesema mwaka wa fedha 2022/23 na 2023/24, Serikali kupitia fedha za programu za kuimarisha elimu ya Awali na Msingi (BOOST) na Sekondari (SEQUIP) pamoja na fedha za Serikali Kuu, imejenga nyumba 860 za walimu wa shule za msingi na sekondari zitakazochukua familia 2,018.
Amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia programu za miradi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu ili walimu wapate mahali bora pa kuishi.
Kadhalika Jacqueline amehoji Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo unaenda kwa kasi na ina mpango gani wa kuyapa kipaumbele maeneo ikiwamo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali inatambua mahitaji ya miundombinu ya elimu, hivyo imekuwa ikiwashirikisha wananchi kupitia halmashauri katika ujenzi wa nyumba za walimu.
Amesema hadi sasa imepokea maboma 2,470 ya nyumba za walimu na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuunga mkono jitihada za wananchi.
Amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri wafanye tathimini ya maboma hayo.