KATIKA Makao Makuu ya Klabu ya Yanga SC, unaweza kusema hakuna kulala kwani mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wameendelea kufanya amsha-amsha kama hamasa ya kuelekea Kariakoo Dabi itakayochezwa Aprili 20, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa.
Yanga ni mwenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, ndiyo sababu ya mashabiki wa Yanga kutoka matawi mbalimbali yaliyopo Dar es Salaam, kukusanyika katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa mashabiki maarufu wa klabu hiyo anayejulikana kama ‘Mzee wa Utopolo’, amesema lengo la kukusanyika klabuni hapo ni kuanza safari kwenda Kigamboni ilipo kambi ya timu hiyo.
“Vaibu letu tumelianza mapema kwa sababu mechi yetu imekabidhiwa kwa wazee wetu ndio maana tutakapofika Kigamboni, tutapokewa na wazee,” amesema na kuongeza;
“Kesho tena tutakutana hapa, kisha tutaenda kumalizia Manzese ambako pia tutapokewa na wazee.”
WAZEE WA JANGWANI
Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, Shaban Uda, amemtaka kila mzee wa timu hiyo aiombee kwa imani yake.
“Maana ya viongozi kuikabidhi mechi kwa wazee ni utaratibu, ndio maana wamefanya kwa Aziz Ki, Pacome, Maxi Nzengeli, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya… ni namna gani wanaonyesha kuheshimu watu,” amesema na kuongeza:
“Ikiwa hii ni Wazee Day, sisi tunasema hakuna vazi maalum kama ilivyokuwa Bacca Day walivaa msuli, Pacome Day waliweka ‘bleach’, sisi tumewaambia watu wavae kiheshima kwa sababu wazee tuna heshima yetu.”
Timu hizo zinakutana huku Yanga ikiwa na morali zaidi hasa baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa pia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, mwaka jana kushinda mabao 5-1.
MWENYEKITI MATAWI HUYU HAPA
Mwenyekiti wa Matawi ya Wanajangwani Mkoa wa Dar es Salaam, Shaban Uda amesema kwa kuwa wazee kutoka kwenye matawi yao wanashauriana namna gani ya kuhakikisha mechi yao ya Jumamosi dhidi ya watani wao Simba wanashinda.
“Tunaiheshimu Simba, tunaambiana hatuwezi kwenda kwa kuizoea licha ya kuifunga mabao 5-1 mzunguko wa kwanza, hilo halimanishi wana timu mbaya, itakuwa mechi ya ushindani mkali,” amesema na kuongeza;
“Kitu kingine tunachokifanya tunahamasishana siku ya mechi tujitokeze kwa wingi ili wachezaji wetu wakituona wapate morali ya kujituma na wajue tupo pamoja nao.”
Amesema kama mwenyekiti kwa sasa anatembea kwenye matawi mbalimbali, kuona kinachoendelea kuhusiana na mchezo huo.