Netanyahu alemewa na shinikizo kufikia makubaliano – DW – 03.09.2024

Kwenye hotuba yake kwa taifa kufuatia maandamano na mgomo mkubwa siku ya Jumatatu (Septemba 2), Netanyahu alisema ameziomba radhi familia za mateka sita ambao miili yao ilipatikana mwishoni mwa wiki kwenye Ukanda wa Gaza, lakini wakati huo huo alisisitiza kuwa asingeliweza kufikia makubaliano yoyote na kundi la Hamas ikiwa kundi hilo halitatimiza masharti ya serikali yake inayofuata siasa kali za mrengo wa kulia.

“Niliziambia familia hizi na nasema tena jioni hii: Naomba msamaha kwa kushindwa kuwarejesha nyumbani wakiwa hai. Tulikuwa karibu sana na kufanya hivyo, lakini hatukufanikiwa. Na pia nasema jioni hii: Israel haitalikubali hili.” Alisema waziri mkuu huyo.

Soma zaidi:Biden asema Netanyahu anakwamisha mapatano Gaza

Inakisiwa kwa sasa wamesalia mateka 97, wakiwemo 33 ambao wameshakufa ama kuuawa, kwa mujibu wa jeshi la Israel.

Kati ya mateka 251 waliochukuliwa na wapiganaji wa Kipalestina siku ya tarehe 7 Oktoba kutokea kusini mwa Israel, ni wanane tu walioweza kuokolewa wakiwa hai na jeshi la Israel. Wengine pekee waliopatikana salama ni kwa  makubaliano ya kubadilishana mateka mnamo mwezi Novemba.

Hamas yatoa muongozo mpya wa mateka

Msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas, Abu Obeida, alisema kwenye taarifa yake kuwa mateka waliosalia wanaweza kurudi kwenye majeneza endapo Israel itaendelea na operesheni yake ya kijeshi.

Israel Jerusalem | Beerdigung der israelisch-amerikanischen Geisel Hersh Goldberg-Polin
Rais Isaac Herzog wa Israel na mkewe Michal wakihudhuria mazishi ya mmoja wa raia ambao maiti zao zilipatikana kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Gil Cohen-Magen/AFP/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanamgamo wa Kipalestina wanaowalinda mateka hao wamepewa maagizo mapya juu ya nini cha kufanya endapo vikosi vya Waisraeli vimewavamia.

Soma zaidi: Vita Gaza ni mtaji wa kisiasa kwa watalawala wa kikanda?

Kwenye mitaa ya Tel Aviv, maelfu ya raia walimiminika mitaani kumshinikiza Netanyahu na serikali yake kutoiwacha fursa iliyopo sasa ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kurejeshwa nyumbani kwa mateka waliobakia hai kwenye Ukanda wa Gaza. 

Shinikizo lazidi

Waandamanaji hao walibeba mabango yanayosomeka: “Hii ndiyo fursa yetu ya mwisho. Saini makubaliano”, na mengine yakiandikwa: “Tumechoka na serikali hii inayomwaga damu.”

Israel | maandamano Tel Aviv
Maandamano ya kuishinikiza serikali ya Israel kuwarejesha mateka wakiwa salama.Picha: Florion Goga/REUTERS

Hayo yakijiri, Uingereza ilisema hapo jana kwamba itasitisha uuzaji wa baadhi ya silaha kwa Israel, kutokana na uwezekano wa silaha hizo kutumika kuvunja sheria ya kimataifa.

Soma zaidi: Waisraeli waanzisha mgomo wakishinikiza kuachiliwa kwa mateka

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, alisema anasikitishwa sana na uamuzi huo wa London.

Hata hivyo, serikali ya Uingereza imesema usitishaji huo wa mauzo ya silaha haumaanishi kupungua kwa uungaji wake mkono wa dola la Israel.

Huko mjini Washington, Rais Joe Biden alikutana hapo jana na jopo la wapatanishi wa nchi yake wanaoshirikiana na wale wa Misri na Qatar kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuwarejesha mateka walio mikononi mwa wanamgambo wa Kipalestina kwa mabadilishano na wale wanaoshikiliwa na Israel. 

Lakini alipoulizwa na waandishi wa habari ikiwa anadhani Netanyahu anafanya juhudi za kutosha kufikiwa makubaliano hayo, Biden alijibu kwamba: “Hapana!”

Vyanzo: DPA, AP, Reuters
 

Related Posts