KISARAWE WASISITIZWA KUTUMIA WATOA HUDUMA RASMI WA FEDHA

Na. Saidina Msangi, WF, Kisarawe, Pwani.

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti amewaasa watoa huduma za fedha wilayani humo kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kwa kufuata sheria za Serikali ili waweze kutoa huduma za fedha wilayani humo.

Mhe. Magoti ametoa rai hiyo alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha waliofika wilayani hapo kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni awamu ya mwisho ya mfululizo wa programu ya elimu ya fedha kwa umma inayotekelezwa na Wizara ya Fedha.

Alisisitiza kuwa endapo kuna watoa huduma za fedha ambao wanaendesha shughuli zao wilayani humo na hawana leseni wakibainika kutoa mikopo bila kusajiliwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

‘‘Kila mtu afanye kazi kwa kufuata utaratibu hakuna mtu anaweza kupata pesa nje ya utaratibu hivyo taasisi za fedha zinazofanya kazi wilaya ya Kisarawe zihakikishe zimesajiliwa kisheria,’’alisisitiza Mhe. Magoti.

Aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kwani itawasaidia kuepukana na mikopo umiza pamoja na kutambua umuhimu wa kuweka akiba.

Aidha, Mhe. Magoti alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanatumia watoa huduma za fedha waliosajiliwa ili kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi wa wilaya hiyo Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya alisema kuwa Serikali inatekeleza programu hiyo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya fedha kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha.

‘‘Ni lazima kuwa makini sana katika kupanga matumizi ya fedha, hakikisha mapato na matumizi, matumizi yasizidi, kila fedha unayopata tunza asilimia kumi tuwe na utaratibu wa kuweka akiba katika sehemu rasmi kwani akiba haiozi na kuhakikisha kuwa unapochukua mikopo taasisi hiyo imesajiliwa na ina leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania,’’ alisisitiza Bw. Kibakaya.

Aliwasisitiza kuwa wasitumie taasisi ambazo hazijasajiliwa na Serikali ili inapotokea changamoto waweze kupata suluhisho kwani kutumia taasisi ambazo hazitambuliki mwananchi atapoteza haki ya msingi ikiwemo kupewa mkopo bila kufuata kanuni za mikopo ikiwemo riba kubwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti, akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha, Afisa Usimamizi wa Fedha Bw.Stanley Kibakaya kulia akifuatiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe Bi. Bupe Hezron Mwakibete. Kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi Bi. Mary Mihigo, na watumishi kutoka wilaya ya Kisarawe, wakati timu hiyo ilipowasili wilayani hapo kwa ajili ya programu ya elimu ya ya fedha kwa wananchi.

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw.Stanley Kibakaya, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa wilaya ya Kisarawe wakati timu hiyo ilipowasili wilayani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.

Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi wa Wizara ya Fedha Bi. Mary Mihigo, akisisitiza jambo wakati akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa wilaya ya Kisarawe wakati timu ya Wizara ya Fedha ilipofika wilayani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.

Afisa Masoko ns Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS Bw. Rahim Mwanga, akiwaelekeza Bi.Lilian Beda Ndembo (kulia) na Bi.Anjela Yohana, kufungua akaunti za uwekezaji katika mfuko wa uwekezaji wa UTT Amis, baada ya mafunzo ya elimu ya fedha iliyotolewa na watalamu kutoka wizara ya fedha wilayani Kisarawe.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kisarawe wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha waliowasili wilayani hapo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi, katika ukumbi wa halmashauri hiyo, Kisarawe.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Kisarawe -Pwani)

Related Posts