Serge Pokou aichongea Simba CAF

WAKATI Simba ikianza kushika kasi, Winga wa Al Hilal, Serge Pokou ameichongea timu hiyo kuelekea mchezo wa mzunguuko wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.

Simba itaanzia ugenini Libya kati ya Septemba 13-15, kisha itarudi nyumbani kwa mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa kati ya Septemba 20-22.

Staa huyo ameifunga Simba mara mbili akiwa na ASEC katika michuano ya kimataifa na Jumamosi iliyopita na akiitumikia Al Hilal kwenye mchezo wa kirafiki uliomalizika kwa bao 1-1 wikiendi iliyopita Jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa juzi, Pokou aliingia kipindi cha pili na kufunga bao dakika ya 76 baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Simba.

Alisema, ameiona Simba mpya na wana wachezaji bora lakini bado wanahitaji muda kujisuka zaidi. Alieleza kuwa, wakati alivyokuwa nje aliwasoma mabeki wa Simba na kuona makosa yao mengi wakishindwa kucheza kwa maelewano huku wakiacha nafasi kubwa ndio maana alipoingia tu aliwafunga bao la kusawazisha.

“Mabeki wa Simba bado hawajacheza kwa muunganiko mzuri, hivyo kama wakikutana na timu yenye washambuliaji na viungo wazuri basi kuna uwezekano wa kufungwa mabao mengi zaidi kwani wanaacha  nafasi.

“Hata hivyo wana kikosi bora ambacho bado kinaendelea kujisuka, kama watafanikiwa kufika katikati ya msimu basi watakuwa wameshakuwa na muunganiko mkubwa,” alisema.

Simba msimu huu tayari imecheza mechi mbili za Ngao ya Jamii ambapo Nusu Fainali ilifungwa bao 1-0 na Yanga, kisha ikashinda 1-0 dhidi ya Coastal Union katika kuwania nafasi ya tatu.

Baada ya hapo ikaanza ligi na kucheza mechi mbili dhidi ya Tabora United (3-0) na Fountain Gate (4-0) ikifanikiwa kufunga jumla ya mabao 7-0.

Hivyo katika mechi zote za kimashindano msimu huu, Simba imeruhusu bao moja tu dhidi ya Yanga. Ikumbukwe kuwa winga huyo wa zamani wa ASEC Mimosas, alihitajiwa na Simba katika usajili wa dirisha kubwa uliofungwa Agosti 15 mwaka huu lakini dili hilo halikufanikiwa baada ya Hilal kutoa kibunda kizito na kumchukua.

Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuhitajiwa na Simba lakini dili lake halikufanikiwa, ameitaja sababu akisema: “Mabosi wa Simba walichelewa kumaliza dili hilo mapema wakazidiwa na Al Hilal ambao walikuja haraka na fedha na kunisajili, Kocha Ibenge ndiye alimaliza kila kitu baada ya kunipigia simu.”

Related Posts