Mwanza. Vifaatiba na vitendanishi vya zaidi ya Sh100 milioni vimeteketea kwa moto katika Kituo cha Afya Kakobe Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza.
Vifaa hivyo vimeungua moto baada ya jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lenye vyumba kutokana na hitilafu ya umeme usiku wa kuamkia Septemba 2, 2024.
Akitoa taarifa jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Buchosa, Dk Vita Ndohele amesema moto ulianzia chumba cha maabara kisha kusambaa vyumba vingine ikiwamo stoo ya dawa.
“Taarifa rasmi ya kuwepo moto jengo la OPD zilitufikia saa saba usiku wa Septemba 2, 2024 jumla ya vyumba saba vimeathirika. Jengo la chumba cha maabara na mali zake zote vimeteketea kwa moto, pia chumba cha dawa kimeteketea kwa moto ingawa baadhi ya dawa chache ziliokolewa kwa kushirikiana na wananchi,” amesema Dk Ndohela.
Amesema tathimini ya haraka imeonesha jumla ya vifaatiba na vitendanishi vyenye thamani ya Sh100 milioni vimeteketea na moto katika chumba cha maabara, huku tathimini ya uharibifu katika chumba cha dawa bado haijakamilika kwa kuwa nyaraka zote muhimu zimeteketea kwa moto huo.
“Jengo la OPD la wagonjwa wa nje, miundombinu yake yote pamoja na samani imeharibika sana na kuhitaji ukarabati mkubwa au ujenzi,” ameeleza Dk Ndohela.
Amesema ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma, ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Buchosa baada ya kubainisha hasara na upotevu wa mali imetafuta vifaatiba vya maabara na dawa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Buchosa na vituo vya afya ili kurejesha baadhi ya huduma, kutumia miundombinu iliyobaki katika kituo hicho kutoa.
“Huduma za afya ya msingi zitaendelea kutolewa ingawa huduma za upasuaji zitarejea baada ya siku nne,” amesema Dk Ndohela.
Diwani wa Kazunzu, Boniface Maseswa amesema kituo hicho kinachohudumia zaidi ya wananchi 20,000 kilikuwa kimewekwa kwenye bajeti ya mwaka 2024/25 kwa ajili ya kupatiwa na Serikali Sh250 milioni ya ukarabati wa miundombinu ikiwamo ya maji.
Naye, Mtanda amemuagiza katibu tawala wa mkoa huo, Elikana Balandya kuunda timu maalumu ya kuchunguza chanzo cha moto huo ndani ya siku 14.