Fei Toto anatoa msimamo Azam FC

KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema licha ya kuondolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu lakini ana imani kubwa na timu hiyo kutokana na kuwa na kikosi bora chenye ushindani, hivyo wanapambana mwakani warudi tena kimataifa.

Azam FC imeondolewa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya APR kutoka Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya nyumbani kushinda 1-0 kisha ugenini kupokea kichapo cha mabao 2-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto alisema kutolewa Ligi ya Mabingwa sio mwisho wa timu yao kuendelea kuonyesha ushindani kwenye michuano iliyobaki huku akibainisha haikuwa bahati kwao kutinga hatua inayofuata.

“Hakuna mchezaji ambaye alitamani tuishie njiani, tulikuwa na malengo makubwa lakini imeshatokea, hatujakata tamaa, tutapambana kuhakikisha tunaipata tena nafasi hiyo msimu ujao na hilo linawezekana kwa sababu tuna kikosi kizuri,” alisema na kuongeza.

“Hata timu ambazo zimekuwa zikifika mbali zilianza kama sisi na kuna timu licha ya ukongwe wao kwa kushiriki michuano hiyo hazijawahi kutwaa mataji, hivyo mwanzo ni mgumu, naamini tukirudi tena hatuwezi kurudia makosa.”

Fei Toto alisema makosa machache waliyoyafanya ndio yamewaondoa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, sasa wanarudi kupambania Ligi Kuu Bara kwa kuhakikisha wanatwaa taji hilo na Kombe la Shirikisho (FA).

“Kupoteza nafasi ya kuendelea Ligi ya Mabingwa kumetupa hasira ya kupambana kusaka nafasi ya kurudi tena kwa kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa Ligi Kuu na hili linawezekana, sisi kama wachezaji tumekubaliana kupambania nembo ya timu yetu,” alisema.

Akizungumzia maisha yake ndani ya Azam FC, Fei Toto alisema anayafurahia kwa sababu yamekuwa yakimjenga kwa kumtoa sehemu moja kwenda nyingine na anatamani kuona anaendelea kuwa bora.

“Nipo kwenye timu sahihi, sijawahi kujuta kujiunga hapa na kitu kikubwa zaidi ambacho kinanifurahisha ni namna ambavyo nimekuwa nikiimarika na kuwa mshindani wa wengine, hili linanijenga na kuniaminisha kuwa naweza kufanya mambo makubwa zaidi nikiwa Azam FC,” alisema.

Azam iliyoanzishwa mwaka 2004, imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili 2015 na 2024 ambapo zote ikiishia hatua ya awali. Pia timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja msimu wa 2013/14, imeshiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa misimu nane huku ikiwa bado haijafanikiwa kutinga hata hatua ya makundi kipindi chote hicho.

Fei Toto akiwa bado anawaza kurudi tena kimataifa akiwa na kikosi cha Azam huku akipania kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, ni wazi amezitangazia vita Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipokezana ubingwa huo tangu mwaka 2001.

Related Posts