Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imetoa siku 21 kwa mtangazaji Burton Mwijaku, kuwasilisha utetezi wake mahakamani hapo.
Mwijaku amefunguliwa kesi ya madai na mchora katuni Ally Masoud, maarufu Kipanya akitakiwa kulipa Sh5.5 bilioni kwa madai ya kumkashifu kupitia mtandao wa kijamii.
Hata hivyo, Mwijaku kupitia wakili wake, Patrick Maleo, ameiomba Mahakama hiyo imuongezee muda ili aweze kuwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi kujibu madai ya Kipaya.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Septemba 3, 2024 na Jaji David Nguyale anayesikiza kesi hiyo.
Jaji Nguyale ametoa maelekezo hayo, wakati shauri hilo lilipotajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, baada ya waleta maombi kudai wajapatiwa majibu na Mwijaku.
Kipanya amefungua kesi hiyo ya madai namba 18911 ya mwaka 2024, Agosti 5, 2024 akiomba nafuu 12 ikiwamo kulipwa fidia kwa kukashifiwa mtandaoni na Mwijaku.
Katika nafuu hizo, Kipanya ambaye ni mtangazaji wa Clouds Media Group (CMG) anaomba alipwe fidia ya Sh5.5 bilioni kutoka kwa Mwijaku kwa madai ya kumshushia hadhi na heshima yake kupitia mitandao ya kijamii.
Leo Jumanne, Kipanya kupitia wakili wake kutoka Kampuni ya Haki Kwanza Advocates, Alloyce Komba amedai shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa lakini hawajapatiwa majibu na mjibu maombi.
Wakili Komba baada ya kueleza hayo, wakili wa Mwijaku, Patrick Maleo amedai mteja wake amechelewa kuleta majibu kwa sababu alikosa wakili.
“Ni kweli mteja wangu alipokea wito wa madai na kwa kuwa alikuwa hajapata wakili, akachelewa muda wa kuwasilisha majibu,” amedai Wakili Patrick.
“Baadaye amenitafuta mimi, hivyo naomba niongezewe muda wa kuwasilisha majibu ya utetezi, halafu Mahakama iendelee na utaratibu mwingine,” amedai Patrick.
Wakili Patrick baada ya kueleza hayo, Jaji Ngunyale amemuuliza wakili Komba iwapo anakitu cha kuongea kuhusiana na majibu ya wakili wa Mwijaku.
Wakili Komba amedai hana pingamizi juu ya kuongezewa muda kwa mjibu madai.
Jaji Ngunyale baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, ametoa siku 21 Mwijaku awe amewasilisha majibu yake mahakamani na kuwapatia waleta maombi katika shauri hilo.
“Mahakama inakupa siku 21 kuanzia leo, uwe umewasilisha majibu ya utetezi na uwe umewapatia pia nakala upande wa pili,” amesema Jaji Ngunyale na kuongeza:
“Na kesi hii naiahirisha hadi Septemba 24, 2024 kwa ajili ya kupanga utaratibu mwingine wa usikilizwaji,” amesema Jaji Ngunyale.
Hata hivyo, mleta maombi (Kipaya) na mjibu maombi (Mwijaku) hawakuwepo mahakamani hapo wakati shauri hilo lilipotajwa, badala yake waliwakilishwa na mawakili wao.
Katika kesi ya msingi, Kipanya amemshtaki Mwijaku kwa kumkashifu kwa maandishi Juni 4, 2024 kupitia ukurasa wake wa facebook wenye utambulisho namba 108657908847651 na kwenye akaunti yake ya Instagram aliandika maneno ya uongo yenye nia ovu na kumfedhehesha yakiwamo kwamba yeye KP (Kipanya) anafanya biashara haramu inayoharibu maisha ya vijana wengi nchini.
Katika hati hiyo ya mashtaka, Mwijaku anadaiwa kuandika kwenye akaunti za mitandao tajwa kwamba Masoud huwazodoa na kuwadhalilisha viongozi wa nchi na Serikali hususani marais kwa kuhongwa.
Kipanya anadai kuwa maneno hayo ya uongo na yenye nia ovu yaliyochapishwa mitandaoni na kusomwa na watu wengi ndani ya jamii na duniani yametafsiri kwamba yeye KP sio mtu mwenye tabia nzuri wa kupewa heshima yoyote kwani hafai, anajihusisha na biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za Serikali au magendo.
“Hivyo kipato chake kinatokana na biashara hiyo haramu na sio uchoraji katuni, utangazaji, ubunifu, ubalozi wa masuala ya kijamii, ukurugenzi wa bodi za taasisi mbalimbali kitaifa na kimataifa,” inadai sehemu ya hati ya mashtaka.
Kutokana na maneno aliyota Mwijaku kwenye mitandao ya kijamii, wakili Komba, ameyachambua katika vipengele 15 akifafanua maana ya maandishi ya Mwijaku kwa tafsiri ya watu wa kawaida ndani ya jamii kwamba mteja wake anaonekana ni mla rushwa, jambazi, tapeli, laghai, asiyeaminika, chanzo cha vijana walioharibikiwa maisha yao.
Pia, mteja wake hapaswi kuhusishwa katika masuala yoyote ya kijamii ikiwamo kupewa fursa na kufanya kazi na taasisi za Serikali ambazo amekuwa akijihusisha nazo katika elimu na malezi ya vijana mashuleni na mitaani.
Katika maombi 12 aliyoomba kipanya dhidi ya Mwijaku ikiwemi kulipwa fidia za Jumla ya Sh5.5 bilioni, Wakili Komba anadai kuwa.
“Kutokana na maandishi ya kashfa ya meneno ya uongo aliyotoa Mwijaku na kunukuliwa alikiri na kuomba radhi mbele ya vyombo vya habari Juni 13, 2024 bila kuchukua hatua ya dhati ya kumsafisha kimaandishi Masoud Kipaya, imeathiri kiajira, kibiashara, kimahusiano ndani ya jamii ya Tanzania kuanzia kwenye familia yake, kisaikolojia na kumshushia hadhi na hesima aliyoijenga kwa zaidi ya miaka 35,” amedai Wakili Komba.
“Hivyo mteja wangu anaomba Mahakama imuamuru Mwijaku, amlipe fidia ya Sh500 milioni ya madhara halisi (specific damages) atakayothibitisha kwa ushahidi mahakamani kutokana na kashfa hiyo na fidia ya madhara ya jumla(General damages) yatakayopimwa na kuridhiwa na Mahakama kwa mamlaka yake ya Sh5 bilioni,” amedai Wakili Komba.
Pia, wakili Komba amedai kuwa mteja wake, ameomba malipo ya kiadhabu kwa mdaiwa yaani Punitive damages na malipo ya fidia ya madhara halisia yaambatane na riba ya asilimia 31 tangu kashfa ilipotolewa yaani Juni 4, 2024 hadi utekelezaji wa hukumu utakapokamilika.
Vile vile Kipanya anaiomba Mahakama katika hukumu yake, itamke kwamba maneno yaliyoandikwa na kusambazwa na Mwijaku yalikuwa ni ya uongo, yenye nia ovu na kuharibu hadhi na heshima yake.
Kipanya, anaoimba Mahakama iamuru Mwijaku kuomba radhi bila masharti yoyote na kuondoa mitandaoni maneno ya kashfa yaliyoandiskwa na kusambazwa.
Lakini pia, Kipanya anaiomba Mahakama itamke na kumuamuru Mwijaku, wakala wake, wasaidizi wake na mtu mwingine yoyote aliye katika mamlaka yake kutosambaza maneno hayo ya uongo na kashfa dhidi ya Masoud Kipaya.
Mbali na maombi hayo, Kipanya pia ameomba kulipwa gharama ya kesi kutokana na kuweka mawakili na nafuu nyingine ambazo Mahakama itaona ni haki na zinafaa apewe.