‘Mifumo itumike kupambana dawa za kulevya Afrika’

Unguja. Ili kufikia malengo ya pamoja katika kupambana na dawa za kulevya nchi za Afrika zimetakiwa kuimarisha mifumo ya kupeana taarifa, kubadilishana mbinu bora na kuongeza ushirikiano kuanzia ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Wakati mapambano hayo yakifanyika, pia nchi husika zinapaswa kuwa na sera na sheria zinazozingatia haki za binadamu.

Hayo yamebanishwa leo Jumanne, Septemba 3, 2024 katika mkutano wa tatu wa Kamisheni ya Kupambana na Dawa za Kulevya kwa nchi zilizo Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESACD) uliofanyika Unguja, Zanzibar na kuwashirikisha wataalamu, watunga sera na viongozi wa Serikali kutoka mataifa hayo.

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo wa siku mbili ni Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Kgalema Motlante ambaye pia ndiye mwenyekiti wa ESACD.

Wengine ni Rais mstaafu wa Mauritius, Kassam Otem ambaye ni kamishna wa tume na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano ambaye ni katibu wa tume.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla aliyemwakilsha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ili kufikia ushindi wa vita ya dawa za kulevya wanapaswa wote waendelee kutekeleza mikakati ikiwamo ya kujikita katika kinga na kutambua viashiria vya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

“Sisi kama wadau tunalazimika kuongeza mapambano haya na kuandaa ajenda mahususi za kutekeleza mikakati ya pamoja na kufanya kazi pamoja huku tukijikita katika kuzuia upatikanaji wa dawa za kulevya na kuimarisha mifumo, ushirikino katika ngazi zote,” amesema.

Amesema jitihada za Tanzania kupambana na dawa za kulevya zimekuwa zikichukuliwa pande zote mbili za Muungano kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria za dawa za kulevya sheria namba tano ya mwaka 2015 na sheria namba nane ya mwaka 2021.

Amesema kwa upande wa Tanzania bara kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi Aprili mwaka huu wamefanikiwa kukamata bangi tani 1,971.9, mirungi tani 337.7 heroine kilogramu 3,536, cocaine kilogramu 61.5 na aina ya methamphetamine kilogramu 2,936.49 kiasi.

Tanzania inatambua sera madhubuti yenye kutoa miongozo ya sheria, tiba, elimu na yenye kuanisha miongozo ya ujumuishi na ushirikiano.

Mamlaka ya Kudhibiti na Dawa za Kulevya Zanzibar imekamata kilogramu 1355.62 zilizihusisha watuhumiwa 518 wakiwamo wanaume 487 na wanawake 31.

Pia imetaifisha mali zitokazo na dawa za kulevya zenye thamani ya Sh15.33 bilioni yote haya ni utekelezaji wa sheria.

Amesema kwa upande wa Tanzania bara kwa mwaka 2023 waraibu 433,062 kati yao 324 wanaume na wanawake 432, 738 wamesajiliwa na kupatiwa matibabu katika vituo vya afya ya akili huku Zanzibar kituo hicho kimesajili waraibu 449.

Rais mstaafu wa Afrika Kusini na Mwenyekiti wa Tume ya Kupambana na Dawa za kulevya, Kgalema Motlanthe amesema wamekubaliana wakati wakiendelea na mapambano hayo lazima kuzingatia haki za binadamu.

Motlanthe amesema pia ipo haja ya nchi husika kuhakikisha zinafanyia marekebisho ya sera na sheria zake ili takwa hilo litekelezwe kikamilifu.

“Sera tulizonazo zinavyotumika kupunguza maumivu badala ya kuongeza kwa watu wanaopatikana na matumizi ya dawa lakini kutenda haki kwa wanaotumia na kuhusishwa katika biashara ya dawa hizo,” amesema.

“Tunaamini Serikali zetu zitazingata masuala haya na kuweka mipango madhubuti kuhakikisha jambo hili tunapambana nalo kwa njia ambazo zinalenga kudhibiti masuala ya usafirishaji na matumzi ya dawa za kulevya katika ukanda wetu wa Afrika,” amesema.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu wa Tanzania, Dk Jimy Yonaz amesema Tanzania imeathiriwa zaidi na dawa za kulevya hususani heroine.

Amesema nchi za mashariki mwa Afrika umekuwa ushoroba wa kupitisha dawa hizo kutoka nchi za Kusini mwa bara la Asia kwenda nchi za Ulaya, Australia na Marekani, hivyo baadhi ya dawa hizo hubaki nchini na kutumiwa na vijana.

Hata hivyo, amesema mapambano hayo yanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya akili mnemba hivyo ipo haja ya kuangalia namna ya kuendelea kupambana na jambo hilo.

Kamishna wa Afya Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii Umoja wa Afrika (AU), Minata Samata Cessouma amesema usafirishaji wa dawa za kulevya hauna mipaka kwa hiyo lazima washirikiane kupambana.

Amesema kwa pamoja wanaweza kupambana na kutokomeza janga hilo barani  Afrika na kwa mataifa yao huku akisisitiza haja ya kuendelea kujengeana uwezo na kufanya operesheni katika mipaka.

Mwakilishi kutoka Mikataba ya Kimataifa ya Kikanda na Changamoto, Huduma kwa Hati za Sera za Kigeni Tume ya Ulaya, Maria Lossa Sabbatelli amesema wanaamini katika kufanya kazi pamoja na kubadilisha uzoefu itasaidia katika kupambana na dawa hizo.

Amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kusaidia katika kuboresha ulinzi wa bahari na kufanya operesheni za mara kwa mara huku kukiwa na sera nzuri zitakazosaidia kuondosha changamoto hiyo ambayo sio tu tatizo kwa Afrika bali ni tatizo la kidunia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Harusi Suleiman amesema mkutano huo wanatarajia utaleta mabadiliko makubwa katika kupambana na dawa za kulevya.

Amesema Zanzibar wamepiga hatua kubwa kupambana na dawa kwa kuboresha sera sheria na mikakati mbalimbali.

“Kwa upande wa sera tumebadilisha na kuona inafaa na inakwenda na wakati kwani tunajua kuwa ni nguzo muhimu huku tukitunga sheria na kudhibiti dawa za kulevya na haki ikiendelea kutendeka.

“Wanaokumbwa na dawa wanapata matibabu na msaada ndipo ikaanzisha kituo cha marekebisho ya tabia kwa watu waathirika ambao wapo tayari kuacha kwa hiari zao,”amesema Suleiman.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni amesema:“Tatizo hili ni kubwa na tishio limeathiri nguvu kazi ya Taifa kwani vijana wengi wandhoofika mwili na akili, kwa hiyo hapa tunazungumza hatima ya vizazi vyetu lakini jitihada zinazidi kuchukuliwa.”

Related Posts