Dar es Salaam. Video zenye maudhui ya kejeli zinazotolewa na Mchungaji Domique Dibwe maarufu kama Kiboko ya Wachawi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zimeibua mjadala huku wadau wakitaka waumini wajihadhari na imani potofu na Serikali iwalinde dhidi ya imani hizo.
Kiboko ya Wachawi aliondoka nchini, baada ya Serikali kulifunga Kanisa la Christian Life Church alilokuwa akiliongoza nchini.
Katika moja ya video hizo, Kiboko ya Wachawi ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), anaonekana akihesabu fedha, huku akisema bado anakumbuka Sh500,000 alizokuwa akiwatoza waumini wake, ili awaombee.
Julai 25, 2024 Serikali ililifungia kanisa hilo lililokuwa Buza, wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam likidaiwa kukiuka taratibu za usajili. Kwa sababu hiyohiyo, Serikali ilifuta usajili wa kanisa hilo.
Katika barua ya kufutwa usajili wa kanisa hilo iliyotolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ilitaja suala la kutoza fedha kuanzia Sh500,000 kwa waumini ili awape huduma ya uponyaji wa kiroho, akisema inakiuka matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019.
Mbali na kutoza fedha, sababu nyingine za kufutwa usajili wa kanisa hilo zilizotajwa katika barua hiyo ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.
Baada ya kufungwa kwa kanisa hilo, mchungaji huyo aliondoka nchini kurudi kwao DRC tangu Julai 29, 2024.
Akizungumza Agosti mosi, 2024, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Paul Mselle alisema uwepo wa kiongozi huyo nchini umekoma baada ya kufutwa usajili wa kanisa lake.
Katika video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mchungaji huyo akiwa Lubumbashi, DRC akieleza maisha yanaendelea akieleza anayekwenda kutafuta miujiza kwake aende na fedha.
Mbali na hiyo, nyingine inamuonyesha akiwa kwenye uwanja unaojengwa kanisa lake mjini Lubumbashi akisema: “Shalom, siku hizi naitwa nabii kero. Tuko site tayari nilikwambia tunajenga hekalu la bilioni nne (Sh4 bilioni). Mungu ametupa neema ya kupata uwanja mkubwa hapa Lubumbashi na kama unavyoona, tunafanya hizi kazi bila kuomba msaada wa mtu.”
Akimwelekeza mpigapicha kuonyesha magari yenye namba za Tanzania anasema: “Si unaona hivyo vyuma vina plate number za Tanzania? Maana yake bado Tanzania nawakubali (anacheka). Mtajua hamjui, wendawazimu.”
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Septemba 3, 2024, Dk Emmanuel Mallya, Mhadhiri Mwandamizi, Sayansi ya Jamii, Utawala na Maendeleo, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), ameishauri Serikali kuwalinda wananchi na imani za dini kama inavyowalinda kwenye bidhaa na usalama wao.
“Kwanza tunaipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya kuwadhibiti viongozi wa dini wa aina hii na kuwalinda wananchi wake, lakini tuendeleze juhudi hizo ili mambo yasifikie huko ambako sasa wananchi wa hali ya chini wanaweza kutapeliwa fedha zao.
“Kama ilivyo kwenye benki au kwenye bidhaa na huduma nyingine, Serikali inapaswa kuwalinda wananchi wake ambao ni wateja au walaji, waumini ni walaji wa imani inayohubiriwa,” amesema.
“Wengi wao hawana uelewa wa kutosha, hivyo taasisi za dini ziwe zinakaguliwa mara kwa mara, hasa hizi ambazo ziko chini ya mwavuli wa mtu na pia zinaongozwa na wageni,” amesema.
Ameshauri kuwapo kiwango cha chini cha elimu ya dini kwa mtu anayefungua huduma ya kidini nchini.
“Pia kuwe na mchakato wa kuchunguza mienendo ya mtu anayeomba kutoa huduma za kiimani, ili kujua kama tabia yake inaendana na miongozo ya Serekali na tamaduni zetu. Lazima tujue kuwa hata mambo ya udhalilishaji yanaweza kutokea kwa watoa huduma za kidini wasio na maadili,” amesema.
Askofu Dickson Kaganga wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) mjini Zanzibar, amewataka waumini kujua wanachoamini na kuwa na uwezo wa kupambanua imani hizo.
“Kwanza waumini wanatakiwa kujua wanaamini nini, kwa sababu usipojua itakuwa rahisi sana kuyumbishwa. Pia muumini anatakiwa awe na uwezo wa kupambanua kwa sababu imani si kuamini vitu vya kijinga visivyo na mantiki,” amesema.
Ametaja uvivu wa waumini, akisema baadhi huamini kupata mafanikio kwa kuombewa.
“Mtu anaamini anaweza kupata mafanikio kwa kwenda kwa nabii, amtabirie ampe mafuta, sasa ukiwa na imani kwamba utapata vitu bure, wewe ni rahisi sana kutapeliwa,” amesema.
Amewataka waumini kuzijua fikra za kishirikina, akisema wapo wanaoamini anaweza kupeleka Sh10,000 zikageuka kuwa Sh1 milioni, au kuamini zinaweza kutoka benki zikaingia kwenye simu.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.