WAKATI Coastal Union ikiendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya mezani kwa mabosi wa kikosi hicho kuna majina mawili ambapo kama yaatapita basi kuna uwezekano wakawa ni kocha mkuu na msaidizi wake.
Taarifa za ndani ya kikosi hicho zimelidokeza Mwanaspoti kuwa klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na makocha wawili ambao wamefundisha timu za Ligi Kuu.
“Majini hayo ni Moalin (Abdihamid) wa KMC anayetakiwa kama kocha mkuu na Zuberi Katwila kama kocha msaidizi. Tunataka kupata uhakika wa watu hao wawili wiki hii ili waingie kikosini haraka,” kilisema chanzo.
Hayo yote yanatokea baada ya wiki chache tangu Coastal Uniao iachane na kocha David Ouma.
Hivi karibuni Mwanaspoti lilitaarifu kuwa, kocha Domonique Niyonzima ni mmoja wa makocha wanaosimamia mazoezi ya kikosi hicho kambini, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Licha ya kwamba mabosi wa Coastal hawajasema lolote juu ya kocha huyo ambaye ni mshauri wa Ufundi wa Fifa kwa nchi za Magharibi, lakini Niyonzima ana wiki kama moja sasa akiwa anahudhuria mazoezi ya timu.
Chanzo kimeeleza Coastal inasikilizia ili kuwa na uhakika wa kuwa na Moalin pamoja na Katwila ili waendeleze alipoishia Ouma.
“Sasa tunahitaji makocha watakaoendeleza alipoishia kocha aliyepita ili timu iendelee na makali kabla ligi haijachanganya, licha ya kuwa tumetolewa katika michuano ya kimataifa,” kilisema chanzo.
Ouma aliifanya imalize nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kukata tiketi ya CAF, huku pia ikifika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na kupoteza mbele ya Azam FC.
Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya Joseph Lazaro na Ngawina Ngawina na ilitoka na sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya KMC.
Moalin anayeifundisha KMC aliawahi kufundisha Azam FC na msimu uliopita alimaliza na rekodi za kuibakiza KMC katika ligi, huku ikimaliza nafasi ya tano.
Kwa upande wa Katwila alikuwa na msimu dume baada ya kutimuliwa Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja, lakini amewahi kuifundisha Ihefu SC (sasa Singida Black Stars).