Straika KenGold amezea mate kiatu

STRAIKA wa KenGold ya Mbeya, Ibrahim Joshua amesema msimu huu amepanga kufunga zaidi ya mabao 16 na kuwa mmoja wa washambuliaji ambao watakuwa wakipigania kiatu cha ufungaji bora Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita kiatu hicho kilichukuliwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI.

Joshua ambaye alikuwa nje ya uwanja msimu uliopita akiuguza majeraha ya goti ana rekodi ya kufunga mabao 16 msimu wa 2021/2022 katika mashindano yote akiwa na Tusker ya Kenya ambayo aliisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya.

“Nina furaha kurudi tena uwanjani na timu ambayo niliipambania nyuma katika harakati za kucheza Ligi Kuu kabla ya kupata fursa ya kwenda Kenya kucheza soka la kulipwa,” alisema.

“Bahati mbaya tumeanza msimu kwa kupoteza, lakini naamini tunaweza kufanya vizuri katika michezo ijayo. Kama mshambuliaji nachohitaji ni kufunga ili kuisaidia timu yangu kufanya vizuri msimu huu.

“Nimejiwekea malengo ya kufunga zaidi ya mabao 16 niliyofunga katika msimu wangu wa kwaza Kenya, naamini huu utakuwa msimu mzuri kwangu maana msimu uliopita ulikuwa mgumu sana kutokana na kusumbuliwa na majeraha.”

KenGold ikiwa nyumbani ilichapwa katika mchezo wa kwanza wa ligi na Singida Black Stars kwa mabao 3-1, bao la kufutia machozi kwa wenyeji likifungwa na Joshua baada ya pasi nzuri kutoka kwa Herbert Lukindo.

Joshua aliyecheza Tusker misimu miwili, wa kwanza akionekana kuwa moto akifunga mabao 16 huku ule wa 2022/23 akimaliza na mabao saba ndiye mshambuliaji kinara KenGold ambao mchezo ujao watacheza ugenini dhidi ya Fountain Gate.

Related Posts