Dar es Salaam. Wanamtandao wa kupinga na kupambana na rushwa ya ngono, wamelipongeza Bunge la Tanzania na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kutopitisha kifungu cha 10 (b) na kuacha kama kilivyo kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Ngono.
Pia, kwa kuongeza wigo wa ukomo wa adhabu kwa waomba rushwa ya ngono kutoka miaka mitatu hadi 10 na faini ya Sh5 milioni hadi 10 milioni.
Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa uliwasilishwa bungeni Septemba 2, 2024.
Baada ya mjadala bungeni, Serikali ilitangaza kuridhia kukiondoa kifungu cha 10(b) kilicholalamikiwa na wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na wabunge.
Akitoa tamko kwa niaba ya wanamtandao huo leo Jumanne Septemba 3, 2024, Rose Marandu amesema hatua ya Bunge kuridhia kutopitisha kifungu hicho na kuongeza adhabu kwa waomba rushwa ya ngono ni ushindi kwenye mapambano dhidi ya rushwa hiyo.
“Tunawapongeza kwa kutimiza wajibu wao kikamilifu, kwa mujibu wa Katiba yetu na kuweka masilahi mapana ya wananchi mbele, huu ni uthibitisho tosha wa nguvu yetu wananchi na umuhimu wa sauti zetu kama wanajamii katika kukataa mifumo kandamizi,” amesema.
Amesema kifungu cha 10(b), kilichokuwa kimeongezwa kwenye mabadiliko hayo kinahalalisha matumizi mabaya ya mamlaka kwa kuwaadhibu waathirika wa rushwa ya ngono kama mbinu ya kuwatisha.
“Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye amemsababishia mwenye mamlaka kufanya kosa kwa kumuahidi, kumshawishi, au kutoa rushwa ya ngono ili apendelewe, apewe cheo, ajira, au kupandishwa cheo, anakuwa hatiani kwa kosa la rushwa ya ngono,” amesema.
Mwanamtandao, Dk Ave-Maria Semakafu ametoa wito kwa jamii kuendelea kukemea vitendo hivyo akisema vina athari katika ustawi wa uchumi na jamii kwa ujumla, hasa kwa waathirika.
Amesema vitendo hivyo vinaathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa Taifa kwa kusababisha matumizi mabaya ya rasilimali watu, hivyo kudhoofisha jitihada za kupambana na umasikini.
“Vitendo hivyo vinahujumu utu wa Taifa kwa kugeuza haki kuwa upendeleo kinyume cha maadili ya utendaji kazi na kinyume cha mikataba na makubaliano ya kimataifa na kikanda yanayokataza vitendo vya rushwa ya ngono,” amesema.
Amesema vitendo hivyo humpokonya na kumdhalilisha mtu utu wake, na kumnyima fursa za kukuza vipaji vyake.