Chadema Mbeya yaja na Operesheni K3 ikijiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa

Mbeya. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, kimezindua operesheni mpya ya K3 wakati kikijiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.

K3 ni kifupi cha maneno “Kujiandikisha, Kupiga kura na Kulinda kura,” huku operesheni hiyo ikiambatana na elimu kwa wafuasi, viongozi na wagombea wa chama hicho kujipanga vema kuhakikisha kinashinda uchaguzi huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Septemba 3, 2024, mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Masaga Kaloli amesema operesheni hiyo itatumika kama salamu ya mkoa katika kujiweka sawa na uchaguzi huo.

Amesema matarajio yao ni kuona Chadema ikishinda ngazi zote kwa kuwa, mwaka huu wamejipanga kiushindani na siyo kulalamika wala kulia kwa madai ya kuibiwa kura na kila ngazi watasimamisha mgombea.

“Hii ni operesheni tuliyopitisha mkoa, tunaendelea kuhamasisha viongozi wa wilaya na majimbo kuandaa watu wenye uwezo na imara ili kila ngazi tuwe na mgombea, mwaka huu hatutaki kulialia kwamba tumeibiwa kura,” amesema Kaloli.

Ameongeza kuwa Septemba 20, 2024 wanatarajia kupokea majina ya wagombea wote na kwamba operesheni hiyo itaambatana na elimu kwa wananchi, wafuasi na viongozi wa chama kuhakikisha wanatimiza haki yao kikatiba.

“Viongozi wa wilaya na majimbo yote wameshapewa maelekezo kusimamisha wagombea wenye kujipigania, matarajio yetu ni ushindi wa kishindo kwa ngazi zote,” amesema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Wazee wa chama hicho, Hugho Kimaryo amesema baada ya kupitishwa operesheni hiyo, wanasubiri elimu kwa kuwa lengo ni kumuweka mwananchi kutambua haki yake.

Amesema Chadema wanatarajia matokeo makubwa ya operesheni hiyo ikiwa ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kupiga kura na kulinda matokeo.

“Hiyo operesheni imezinduliwa jana, sisi wafuasi tunasubiri elimu iwafikie wananchi wote ili tunapoenda kwenye uchaguzi, kila mmoja aijue haki yake Kikatiba, tunatarajia matokeo chanya,” amesema Kimaryo.

Mmoja wa wafuasi wa chama hicho, Hilda Mwalimu amesema iwapo haki itatendeka katika uchaguzi huo, Chadema inakwenda kushinda kutokana na sera walizonazo na matakwa ya wananchi kutaka mabadiliko.

 “Hakuna ambaye hakuona kilichotokea uchaguzi uliopita, lakini kwa mwaka 2024, Chadema itashiriki kikamilifu na tunaamini tutashinda kama hakutatokea figisu,” amesema Hilda.

Related Posts