KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi ameweka wazi kwamba alihusika katika ushawishi wa kumbakisha mshambuliaji Clement Mzize asiondoke klabuni hapo huku akitaja sababu mbili za uamuzi wake huo juu ya kinda huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema licha ya ofa ambazo Mzize zimeanza kutajwa akitakiwa na klabu kubwa za Afrika, lakini bado mshambuliaji huyo anatakiwa kubaki ndani ya timu hiyo ili aweze kujiongezea thamani kubwa sokoni.
Gamondi alisema Mzize bado yupo kwenye timu salama ambayo inaendelea kupiga hatua kubwa kusaka mafanikio makubwa Afrika na inaweza kwenda kufika mbali katika mashindano ya Afrika, na hata kuchukua taji.
Kocha huyo alisema ndani ya kikosi hicho licha ya kuwa na wachezaji wakubwa, Mzize bado amekuwa mchezaji muhimu akipata muda wa kutosha wa kucheza na kukuza kipaji.
“Nadhani nyie waandishi mliwahi kuniuliza kwanini namtumia Mzize badala ya kuwatumia wachezaji wengine wenye uzoefu, niliwajibu lakini mnaweza kuona kazi ambayo anaifanya Mzize akiwa uwanjani,”alisema Gamondi.
“Kuna wakati unahitaji mchezaji mwenye kasi, nguvu na akili ya kusababissha madhara kwa timu pinzani kama Mzize, ndio maana mnaona tumeendelea kumtumia katikati ya wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
“Nikweli nilihusika kumshawishi abaki kwa kuwa hata hapa Yanga ni sehemu sahihi kwake kuendelea kukuwa ili aweze kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi hapa Afrika na hata Ulaya na nawashukuru viongozi wa klabu nao wakafanikisha hilo.
Gamondi alisema mshambuliaji huyo pia klabu imefanya hatua nzuri kumboreshea maslahi hatua ambayo itamfanya kutuliza akili yake kufanya kazi kama ambavyo anafanya sasa.
“Kumwambia kumbakisha na kumpa nafasi peke yake haitoshi, lakini viongozi wa klabu nao wanaona namna anavyoendelea kukua na wakaona ni wakati mzuri kumboreshea maslahi yake ili aweze kuwa na akili iliyotulia, nadhani mnajua soka ni maisha yake.”
Ndani ya mechi tano za nyuma ambazo Yanga imeshinda zote Mzize amefunga mabao matano akiwa ndio mshambuliaji aliyefanya vizuri zaidi ndani ya kikosi hicho cha Yanga.