Ajiua kwa kujinyonga ikidaiwa alifumaniwa akimbaka mjukuu

Dodoma/Moshi. Wakati Serikali, wadau na jamii kwa ujumla ikipambana kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, matukio ya ubakaji na ulawiti yameendelea kuripotiwa katika maeneo kandaa nchini.

Mkoani Kilimanjaro inaripotiwa kuwa, katika Kijiji cha Kifuni, Kata ya Kibosho Magharibi, wilayani Moshi, Wenseslaus Olomi (50), amejiua kwa kujinyonga ikidaiwa ni baada ya kufumaniwa akimbaka mjukuu wake wa miaka sita.

Katika matukio ya hivi karibuni, Mkazi wa Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota mkoani Dodoma, Stephen Damas (38) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti hadi kusababisha kifo cha mtoto wake mwenye umri wa miezi sita.

Hayo yanaripotiwa wakati ambao ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani ya mwaka 2023, iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania na kuchapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha Januari hadi Desemba, 2023 waathirika 15,301 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto waliripotiwa ikilinganishwa na waathirika 12,163 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Idadi hiyo ni ongezeko la waathirika 3,138 sawa na asilimia 25.8, huku makosa yenye idadi kubwa ya waathirika ni ubakaji (8,185), ulawiti (2,382), mimba kwa wanafunzi (1,437), kumzorotesha mwanafunzi kimasomo (922) na shambulio la aibu (396).

Olomi inadaiwa kabla ya kujiua, mke wake alimfumania akimbaka mjukuu wake, hivyo alipiga yowe kuomba msaada ndipo alipomtaka mama huyo aondoke nyumbani na asipofanya hivyo atachukua uamuzi wa kumuua.

Inaelezwa baada ya mke wake kupata vitisho hivyo, aliondoka nyumbani na kwenda kutafuta sehemu nyingine ya kuishi.

Aliporejea Septemba 2, alikuta mlango upo wazi huku mwili wa mume wake ukining’inia juu ya kenchi ya nyumba akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha tukio hilo. Amesema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia.

Mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye ni ndugu wa familia hiyo, Digna Olomi amesema akiwa nyumbani kwake alipata taarifa kuhusu tukio hilo.

“Jana (Septemba 2) nikiwa nyumbani nilipigiwa simu kwamba kuna mtu kajinyonga, hivyo nilimpigia simu diwani na mtendaji nikaenda nao eneo la tukio, tulipofika tulimkuta kajinyonga,” amesema.

Amesema mke wa Olomi alimweleza alifukuzwa na mume wake kutokana na ugomvi kati yao na alimweleza asipomuua atajinyonga, hivyo ikabidi aondoke nyumbani.

Kuhusu taarifa za mwanamume huyo kudaiwa kumbaka mjukuu wake, amesema amezisikia.

“Kuna watu wanasema kuna jambo amefanya ambalo lingemfanya afie ndani (magereza) nikauliza ni nini watu wanasema kwamba amembaka mjukuu wa miaka sita,” amesema.

Katika tukio lilitokea Mbuyuni, Damas anadaiwa kulitenda Septemba mosi, 2024 saa tatu usiku na kisha kutelekeza mwili wa mtoto huyo wa kike nyumbani kwa bibi yake.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 2, bibi wa marehemu, Elizabeth Sudai alidai mkwe wake (Damas) alifika kwake Septemba mosi saa tatu usiku na kumgongea mlango.

“Nilikuwa nimelala, akaniita, mama, mama mjukuu wako huyo hapo. Nikatoka nikakuta mtoto amelazwa kizingitini. Niangalie aliyemleta mtoto, nikaangaza lakini sikumpata,” alisema.

Alisema alipombeba mtoto hakuwa akitikisika bali amelegea hali iliyomfanya kutafuta majirani akawaeleza kilichotokea.

Baada ya kushauriana na majirani, alisema walikwenda kwa balozi na kisha hospitali ilikogundulika kuwa mtoto amefariki dunia baada ya kubakwa na kulawitiwa.

Balozi wa Shina namba tano, katika Mtaa wa Mbuyuni, Tausi Rashid alisema mtoto alipofikishwa kwake, aligundua kuwa hana fahamu, hivyo alipiga simu kwa polisi kata aliyetoa maelekezo waende kituo kikuu cha polisi.

Alisema walikwenda polisi na baadaye hospitali ilikogundulika kuwa mtoto alilawitiwa.

“Nikamuuliza mama yake kama walikuwa na ugomvi, akasema hawakuwa na ugomvi wowote siku ya jana (Septemba mosi) na kwamba baba alimchukua mtoto akawa anacheza naye ndani,” alisema.

Akimkariri mama wa mtoto huyo, Tausi alisema saa moja usiku Septemba mosi baba huyo alitoka na mtoto kama anaelekea dukani, hivyo hakuwa na hofu yoyote.

Tausi alisema saa mbili usiku mama huyo alimtafuta mume wake bila mafanikio hadi baadaye ilipobainika kuhusu tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alisema mtuhumiwa anashikiliwa na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

“Jamii iendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwa masuala haya ya ukatili wa kijinsia na watoto ni mtambuka ili kukomesha ukatili huu,” alisema.

Matukio hayo yameripotiwa zikiwa zimepita siku tatu tangu Bunge lilipopitisha muswada wa sheria zinazohusu ulinzi wa mtoto.

Muswada huo unaosubiri kutiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria kamili uliwasilishwa bungeni Agosti 30, 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima.

Muswada huo unazifanyia marekebisho sheria tatu ambazo ni Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura ya 443, Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.

Miongoni mwa marekebisho hayo ni kuwapo adhabu ya kulipa fidia kwa waathirika, huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ikisema suala la fidia kwa mtoto aliyeathirika na vitendo vya kikatili liwe la lazima kwa atakayetiwa hatia.

Mbali ya hilo, muswada umefanya marekebisho na kuanzisha mabaraza ya watoto katika kila kijiji, kata, wilaya, mkoa na katika ngazi ya Taifa ikiwa na lengo la kuanzisha majukwaa yatakayoweza kujua changamoto zinazowakabili watoto na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji unaofanywa katika jamii.

Dk Gwajima alisema marekebisho yamepanua wigo wa makosa ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kwa kuongeza makosa mengine sita, hatua inayolenga kuongeza ulinzi wa watoto dhidi ya uhalifu wa kingono ambao umeongezeka kwa kasi kutokana na kukua kwa teknolojia.

Related Posts