Petroli, dizeli zashuka bei, soko la dunia likitajwa

Dar es Salaam. Bei ya petroli na dizeli ya rejareja kwa Septemba 2024 imeshuka nchini ikilinganishwa na Agosti, huku sababu kadhaa zikitajwa, ikiwamo kushuka kwa gharama za soko la dunia.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha bei za mafuta kuanzia leo Jumatano Septemba 4, 2024 kwa yanayochukuliwa Bandari ya Dar es Salaam, petroli imeshuka kutoka Sh3,231 Agosti kwa lita moja hadi Sh3,140 Septemba.

Pia, kwa petroli inayochukuliwa katika Bandari ya Tanga, lita moja imeshuka kutoka Sh3,229 Agosti hadi Sh3,141 Septemba na kwa Bandari ya Mtwara pia imeshuka kutoka Sh3,304 Agosti hadi Sh3,142 Septemba.

Kwa upande wa bei ya dizeli, taarifa ya Ewura inaeleza bidhaa hiyo inayopokewa Bandari ya Dar es Salaam bei yake imeshuka kutoka Sh3,131 Agosti hadi Sh3,011 Septemba.

Dizeli inakayopokewa katika Bandari ya Tanga imeshuka kutoka Sh3,138 Agosti hadi Sh3,020 Septemba na Bandari ya Mtwara imeshuka kutoka Sh3,140 Agosti hadi Sh3,021 Septemba kwa lita.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule, imetaja mwenendo wa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kushuka kuwa miongoni mwa sababu ya kupaa kwa bidhaa hizo muhimu katika uchumi.

“Bidhaa za mafuta zinazoagizwa na kupokelewa nchini zinazingatia bei za mafuta yaliyosafishwa (FOB) kutoka soko la Uarabuni. Septemba 2024, bei kikomo za mafuta zimekokotolewa kwa kuzingatia bei za soko la Uarabuni za Agosti 2024.

“Kwa kulinganisha na bei za Julai 2024, bei za Agosti 2024 za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa wastani wa asilimia 7.68, asilimia 6.22 na asilimia 6.20, mtawalia,”imeeleza taarifa hiyo.

Pia, taarifa hiyo imetaja sababu nyingine ni gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) zimepungua kwa wastani wa asilimia 10.55 kwa petroli na asilimia 13.64 kwa dizeli, zimepungua kwa wastani wa asilimia 4.46 kwa petroli na dizeli katika Bandari ya Tanga.

Aidha, zimepungua kwa wastani wa asilimia 14.98 kwa mafuta ya petroli na dizeli katika Bandari ya Mtwara.

Related Posts