Dar es Salaam. Matumizi ya umeme jua kama nishati ya kusukuma maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ni moja ya njia inayoweza kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.
Hiyo ni kutokana na kutohitaji fedha kila siku kwa ajili ya kununua mafuta kwa ajili ya jenereta litakalosukuma maji kwenda kwenye mashamba kutoka kwenye vyanzo, badala yake fedha nyingi itatumika mara moja kwa ajili ya vifaa vya umeme jua.
Ushirika wa wahitimu wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo –Sua (Sugeco) ni mashahidi wa matumizi ya umeme jua katika umwagiliaji.
Waandishi wa habari waliokuwa kwenye mafunzo ya namna ya kuripoti habari za nishati mbadala yaliyotolewa na Taasisi ya African Center for Media Excellence (ACME), walipata fursa ya kutembelea mashamba hayo.
Sugeco ilianzishwa na Dk Anna Temu, mhadhiri wa Sua ikilenga kusaidia vijana na wanawake waliomaliza vyuo ambao wamekosa ajira na hata ambao hawakwenda vyuoni.
Ushirika huo ulianzishwa mwaka 2011 ukichukua wahitimu wa Sua pekee, lakini baadaye fursa ilitolewa kwa vijana wote nchini kutokana na kuwapo kwa uhitaji.
Mtaalamu wa kilimo kutoka Sugeco, Marcelina Lubuva amesema umwagiliaji umewawezesha kulima vipindi vyote vya mwaka badala ya kutegemea mvua.
Amesema awali walitumia gharama kubwa za kununua mafuta kila siku hivyo kuongeza gharama za uzalishaji.
“Tulikuwa tunatumia lita 20 za mafuta kila siku kusukuma maji kwa mwezi ni hela nyingi, tofauti na sasa tuna sola zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa jua wenye nguvu ya kusukuma maji kwa ajili ya kumwagilia mashamba yetu,” amesema.
Iwapo mafuta yangeuzwa Sh3,000 kwa lita moja, kila siku wangetumia Sh60,000 ili kumwagilia mashamba yao ikiwa ni sawa na Sh1.8 kwa mwezi.
Amesema kwa umeme jua, ununuzi wa vifaa na kuvifunga ndiyo gharama kubwa katika kilimo cha umwagiliaji kwa njia hiyo.
Mhandisi wa Kilimo wa Sugeco, Kastuli Dalie amesema eneo hilo limefungwa sola saba, kila moja ina wati 520, ambazo zinawapa uwezo wa kusukuma maji kwenda kwenye bwawa wanalotumia katika kilimo cha umwagiliaji.
Bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi lita milioni nane za maji kwa ajili ya umwagiliaji wa ekari kati ya 20 hadi 25 wanazolima.
Amesema wanategemea vyanzo vitatu vya maji; yanayotoka milimani, kutoka bwawa la chuo ambayo ili kuyapata lazima yasukumwe kwa nishati na wanayosukuma kutoka eneo lao.
“Ikiwa vyanzo vyote vinavyoingiza maji vikikauka, bwawa hili lina uwezo wa kumwagilia mashamba kwa miezi miwili au mmoja na nusu,” amesema Dalie.
Tafiti za matumizi bora ya umeme jua zilizotolewa na ACME zinaonyesha kuwa, sola moja inaweza kusukuma maji zaidi ya theluthi moja ya kiwango kinachohitajika katika mashamba madogo yaliyopo katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Utafiti mwingine uliohusisha wakulima 400 kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania wanaotumia umeme jua kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa kati ya miezi minne hadi mitano unaonyesha namna walivyonufaika.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa ACME, Kanda ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Rachel Mugarura amesema utafiti huo umebaini asilimia 91 ya wakulima waliotumia umeme jua kwa shughuli za umwagiliaji walikiri kupunguza gharama za uzalishaji.
“Asilimia 81 waliona umeboresha maisha yao, hiyo ni kutokana na wao kuzalisha msimu mwingine zaidi badala ya kutegemea msimu wa mvua jambo ambalo liliwafanya kupata mapato zaidi,” amesema.
Utafiti unaonyesha upo uwezekano wa kuwapo mifumo inayotumia umeme jua katika kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa.
Licha ya kuwapo manufaa hayo, wauzaji wa vifaa vya sola wamekuwa wakilazimika kutumia nguvu nyingi kuwashawishi wakulima kutumia umeme jua kama chanzo cha nishati ya kusukuma maji kwa ajili ya kumwagilia mashamba yao.
Hiyo ni kutokana na wengi kushindwa kuamini kuwa umeme huo una nguvu ya kufanya kazi kama ile wanayoweza kuipata katika umeme uliozoeleka au jenereta.
“Wakati mwingine inabidi kutumia mifano hai ili kuwafanya waingie katika kilimo nafuu, utegemezi wa mafuta katika kusukuma maji unaweza kuathiriwa na vitu vingi ikiwemo upatikanaji wake,” amesema Joshua Marco, wakala wa sola.
Alichosema kuhusu bei za mafuta kinaonekana kila mwezi pale Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inapotangaza bei mpya za mafuta kwani kumekuwa na kushuka na kupanda.
Ongezeko la bei za mafuta limekuwa likiathiriwa na vitu mbalimbali ikiwemo bei yake katika soko la dunia.
Matumizi ya umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji yanafanyika katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi ya vikundi vikionyesha ahueni waliyoipata.
Kikundi cha Jitume kinamiliki ekari 26 za umwagiliaji zilizopo katika skimu ya Lupembe Lwasenga, wanakikundi walieleza wanaona ahueni baada ya kuachana na matumizi ya jenereta katika kazi zao.
Imeelezwa kikundi hicho kinaokoa Sh70,000 kila siku zilizokuwa zikitumika kununua mafuta.
Kikundi kingine ni cha Pinos Farm kinachomiliki ekari 16 wilayani Iringa kilichokuwa kikitumia Sh50,000 kila siku kwa ununuzi wa mafuta.
Vikundi hivyo kwa sasa vinatumia umeme jua katika kilimo cha umwagiliaji kwa msaada wa Taasisi ya Elico.