KONA YA MALOTO: Kifua cha Marko Ng’umbi kina mengi kuhusu uhalifu wa kidola

Mwanazuoni wa Ujerumani, Friedrich Nietzsche alishaweka sawa tafsiri kuhusu uhalifu wa kidola, ni makosa yote yenye kufanywa na dola kimfumo au kiongozi mmoja mmoja.
Kutanua tafsiri; vitendo vya rushwa na ufisadi, uharibifu wa uchaguzi na ukandamizaji wa demokrasia, uvunjifu wa Katiba, hata ukiukwaji wa sheria. Makosa yoyote yenye kufanywa serikalini moja kwa moja hubeba mantiki ya uhalifu wa kidola.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marko Ng’umbi, video yake imesambaa mitandaoni, akitamba jinsi Serikali ilivyohusika kufanya uhalifu wa uchaguzi. Marko amejiweka katikati ya muktadha, maana amesema yeye alishiriki.
Marko anasema madiwani waliopita bila kupingwa ulikuwa mpango wa Serikali. Hata kwenye majimbo, Serikali ilihusika, naye alishiriki. Hadi maporini, yaliyotendeka, ulikuwa mpango wa Serikali, naye alishiriki. Hii ni bila kumwongezea maneno.
Rais Samia Suluhu Hassan amemfuta kazi Marko mara moja. Ni jambo jema. Hata hivyo, ukweli dhahiri ni kwamba kifuani kwake inaonekana kuna mengi, ndiyo maana anashindwa kujizuia, kwa hiyo anajikuta anadondosha vingine hadharani, ama kwa kupanga au kutokupanga.
Ukitafsiri maneno ya Marko kwa utaratibu wa kupita katikati ya mstari, utayaona majigambo ndani yake, jinsi mambo yasiyofaa yanavyofanywa kwa masilahi ya wachache kwenye mfumo wa dola. Kwake hiyo ni fahari tena ya uhalifu.
Mfano mzuri ni kashfa ya Watergate, iliyomwondoa madarakani Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nixon mwaka 1974. Hata hivyo, mafanikio kwa jumla yanabebwa na Bunge la nchi hiyo baada ya vyombo vya usalama kuzidiwa nguvu na ushawishi wa Rais.
Kuelekea Uchaguzi wa Rais Marekani, uliofanyika Novemba 7, 1972, Nixon wa Republican akiwa anagombea ili kurejea madarakani kwa muhula wa pili, timu yake ya kampeni ilifanya umafia kwa kuingia kwenye ofisi za Kamati ya Taifa ya chama cha Democrats (DNC), zilizokuwepo kwenye jengo la Watergate, Washington DC.
Timu ya Nixon iliwatumia pia maofisa wa idara za ujasusi za CIA na FBI. Uvamizi huo ulilenga kudukua mawasiliano yote ya kampeni za Democrats kwa kuingiza vifaa vya kunasia mazungumzo kwenye simu, vilevile kuchukua nakala ya nyaraka zote za kampeni.
Uvamizi wa kwanza ulifanyika Mei 28, 1972 na kufanikiwa kuingiza vifaa vya kunasa mazungumzo ya simu, kisha mara ya pili ikawa Juni 17, 1972, wakavunja kabati la nyaraka za DNC, hivyo kunakili siri zote za kampeni za Democrats.
Siku hiyo, Juni 17, mmoja wa walinzi wa Watergate aliona waya uliotumiwa na makomandoo waliofanikisha operesheni hiyo ya kuvamia ofisi za DNC, akaukata bila kutilia shaka jambo lolote. Baadaye mlinzi huyo akawaona makomandoo wakijaribu kuunganisha waya mwingine, hivyo akatoa taarifa polisi. Maofisa wa FBI walifika na kuwakamata watu watano waliokuwemo kwenye ofisi za DNC. Ikabainika watu hao ni makomandoo wa Cuba waliopewa mafunzo Marekani ili kumpindua aliyekuwa kiongozi wa Cuba, Fidel Castro.
FBI walipowapekua makomandoo hao, waliwakuta na vielelezo vyenye kuonyesha wanawasiliana kwa ukaribu na maofisa wa Ikulu, hasa kitengo cha siri cha ujasusi wa kuzuia taarifa nyeti za Serikali zisivuje kwenye vyombo vya habari (White House Plumbers).
Baada ya makomandoo hao kukamatwa, haraka sana Rais Nixon alitumia mamlaka yake kuhakikisha wavamizi hao wa ofisi za DNC hawahusishwi na Republican. Zaidi picha ikageuzwa na kuwa kashfa kubwa kwa Democrats.

Turudi kwa Marko
Yupo mtu aliuliza; je, Rais Samia amemfuta kazi Marko kwa kuzungumza hadharani mambo ya sirini? Mwingine alihoji; 
Rais Samia hapendi Serikali ihusike na uhalifu, ndiyo maana alimtimua Marko?
Jibu lolote lile, mkazo kwa Serikali ni kujiweka kando na uhalifu wa kidola. Hilo haliwezi kufanikiwa kwa kumfukuza kazi Marko, bali kujenga mifumo imara yenye kuaminika ambayo itasimamia uchaguzi wenye sura huru, haki, uwazi, uadilifu na uaminifu.
Kipindi ambacho wapinzani wanalalamika kuibiwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020, Marko anasema yasiyosemwa kuhusu ushiriki wa Serikali kufanikisha uhalifu wa uchaguzi.
Je, Marko ni mwongo? Achukuliwe hatua zaidi. Isiishie tu kumfukuza kazi. Vipi, Marko amekuwa mkweli? Basi hatua zufuatwe ili aseme yote, kisha uwe mwanzo wa kuweka msingi ili matendo ya uhalifu wa kidola kwenye uchaguzi yasijirudie. Isisahaulike, Nixon aling’olewa Ikulu kwa sababu ya uhalifu wa uchaguzi.
Baadhi ya vielelezo vya uvamizi wa DNC vilikutwa Ikulu ya Marekani, White House.
Baraza la Wawakilishi lilipokea ripoti ya Seneti kisha kuungana bunge zima (Congress) na kuandaa hoja ya kumwondoa madarakani Nixon. Agosti 9, 1974, Nixon alijiuzulu na makamu wake, Gerald Ford alimrithi.
Simulizi ya Watergate ni kuonyesha jinsi uhalifu wa kidola unavyokuwa. Ikulu inaweza kuhusika moja kwa moja, kama ambavyo White House, chini ya Nixon, ilivyokuwa. Idara za usalama Marekani zilikuwa zimeshindwa kukata mzizi wa fitina kwa sababu wahusika wa uhalifu walikuwa watu wazito. Baada ya Congress kukamilisha kazi, siyo tu kwamba Nixon alijiuzulu, bali wasaidizi wake wengi walifungwa.

Related Posts