NIKWAMBIE MAMA: Ma-RC, DC punguzeni vioja, mna kazi kubwa ya kufanya

Miongoni mwa makosa makubwa ya wanasiasa ni kudhani siasa ni taaluma kama vile ualimu au uhandisi. Wanadhani ubunge, udiwani, uenyekiti wa mtaa na nafasi nyingine zinatosha kuwafanya waachane na taaluma zao na kushughulika na siasa tu. Kutokana na ugumu wa maisha, watu wengine wanaiona siasa kuwa fursa ya haraka ya kupata mafanikio kwa wepesi kuliko ajira. Wanaigeuza siasa kuwa rungu la kutafutia fedha badala ya kutumikia wananchi.

Dhana hii imewafanya wataalamu kuamini kuwa kuna mtelezo kwenye upande huo. Wanafikia kukwepa taaluma zao na kujichomeka kwenye siasa. Mbaya zaidi, wanapopewa dhamana za kisiasa wanapoteza uelekeo na kuwa mfano wa bendera inayofuata upepo. Hili linatokea kutokana na ukweli kwamba siasa si shamba wala kiwanda, hakuna chakula au fedha zinazozaliwa humo hadi mtu aache kuzalisha mali na kutegemea siasa impatie kila anachotaka.

Mwanasiasa ni mwanadamu kama walivyo wengine. Anahitaji chakula, mavazi, malazi, matibabu, usafiri, kulipa kodi na kusomesha watoto. Hivyo anapaswa kufanya kazi ya kukidhi mahitaji yake kama wafanyavyo wanadamu wengine. Kwenye kazi hizo ndipo atagundua changamoto zinazowakabili watu wake, na bila shaka atashirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi. Akikosa shughuli kama hizo ataishi kwa kurarua kodi za wananchi na fedha za miradi ya maendeleo.

Watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya siasa, uongozi na kazi. Hawa ndio wale ambao mara wakipata nafasi wanauchukulia mdomo kuwa nyenzo ya uzalishaji mali. Wanazalisha maneno mengi yasiyo na msingi wa maendeleo. Adui zake wakubwa watakuwa ni wale waliodanganyika na maneno yake hadi kumwamini, lakini pia atajenga uadui na wenzake wanaopigania maendeleo ya Taifa akichelea kuwa hao ndio watakuokuwa wa kwanza kumuumbua.

Mwanasiasa wa aina hii si mbunifu wa maendeleo. Yeye atakuwa akiota ndoto moja tu: kuteuliwa katika uongozi. Niseme ukweli; mwanasiasa uchwara anaamini kwamba siasa pekee ndiyo nyenzo ya kumfikisha kwenye uongozi. Mungu akimsikia na akateuliwa kuuvaa uheshimiwa, atasahau habari ya kutoka jasho na kuamini kuwa yeye ameumbwa kutoa amri tu. Hatakuwa kiongozi bali mtawala.

Awamu ya kwanza ya uongozi hapa nchini ilijitahidi sana kumtengenezea mwanasiasa chapa ya aina yake. Moja ya masharti ya uongozi ilikuwa ni kutomiliki viwanda wala majumba ya kupanga. Viongozi walishiriki kazi za pamoja na wananchi kama kulima, kufuga, kuvua na kuwinda. Hawakulipwa fedha za ziada kama viongozi, bali waliambulia posho iliyowakimu kwenye mahitaji yao ya msingi. Jambo hili lilisisitiza kwamba uongozi ni wito na si mamlaka.

Haikuwa rahisi kwa mtu ambaye hajaguswa moyoni mwake kuacha kazi iliyompa mshahara na kuingia kwenye siasa. Tunaona wakati Mwalimu anaacha kufundisha na kubobea kwenye harakati za ukombozi. Alilazimika kuchangiwa fedha za kujikimu na waumini wake katika jambo lao. Wanasiasa walijitoa kwa hali na mali kuhakikisha wananchi wanajitawala na kupata haki zao za msingi.

Katika uchaguzi huu wa 2024 na 2025, wapigakura wahakikishe wanawachagua wataalamu wanaoweza kudumu na taaluma zao huko mjengoni. Tuhakikishe hatupeleki wasaka tonge kuanzia mtaani hadi taifani. Huu ni wakati wa Serikali kutumia taaluma za viongozi kukuza uchumi wa nchi. Mawaziri wawe chachu ya maendeleo wakitumia taaluma zao kupitia Wizara husika. Waongeze uelewa wa wananchi kupitia matamasha, semina na makongamano kote nchini.

Sasa tuache kupeana nafasi kwa mazoea, na badala yake tuzingatie taaluma. Kila mtu ana utashi wake, lakini taaluma inaweza kumwondoa yeyote asiishi kwa kuufuata utashi. Watoto pacha wanaweza kufanana tabia, lakini atakayesoma kwenye Chuo cha Seminari hatoweza kuwa sawa na yule atakayesomea CCCP. Kila mmoja wao atakuwa na weledi kwenye mrengo wake.

Hili lizingatiwe hadi huku mikoani, wilayani na mitaani. Sote tunajua kwamba jukumu la kulinda amani na usalama wetu ni la kwetu sote. Lakini kwa sababu wavunjaji wa amani wanakuja na mbinu nyingi, tumewapa dhamana hiyo Jeshi la Polisi chini ya kamanda wao wakuu na Waziri mwenye dhamana kuhakikisha tunakuwa sawa.

Polisi wana taaluma ya kukabiliana na uvunjifu wa amani wa aina zote, ikiwemo ya utumiaji silaha.

Ukitaka kuona kwamba wanasiasa hawajui tofauti ya siasa na taaluma, tazama jinsi Mkuu wa Wilaya au Mkoa anavyoshindwa kuheshimu mipaka yake ya kazi. Ananyosha mkono juu ya wenye taaluma yao na kumuru kwa matakwa yao. Watu wanawekwa ndani huku mamlaka zikishindwa kuamua hatima ya kesi zao.

Wakati mwingine mkuu huyo anaweza hata kuamuru kukamatwa kwa mlinzi wa amani. Kisa, eti yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi.

Hivi Jenerali wa Polisi akiwa Mwenyekiti wa Kamati kuna ubaya gani? Nadhani tumefikia mahala pa kutafakari iwapo wanasiasa wanafaa kuongoza, au wapewe kazi zingine wakati wataalamu wakichukua nafasi.

Je, ni kweli hawaelewi hata hili la dhamana ya kusimamia amani na usalama kuwa ni la watu mahususi kwa shughuli hiyo? Kama ndivyo basi tumo hatarini kupata viongozi watakaoamuru bandari ya Dar es Salaam ihamishiwe Makao Makuu, Dodoma!

Related Posts