Mama afunguka kifo cha mwanaye aliyedaiwa kubakwa na mumewe

Dodoma. Mama wa mtoto aliyedaiwa kulawitiwa na baba yake mzazi hadi kufariki dunia, Stella Gidion amesimulia namna alivyohangaika kumtafuta mwanaye baada ya kuondoka na mumewe.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 3, 2024 nyumbani kwake Mbuyuni, Kata ya Kizota, amesema Jumapili Septemba mosi, baba wa mtoto Stephen Damas (38) aliondoka nyumbani na mtoto akiamini amekwenda dukani.

“Nilikaa hadi saa 2.00 usiku nikaona harudi. Nikamwambia mama mwenye nyumba mbona huyu harudi hadi sasa, ngoja nimfuatilie,” amesimulia.

Amesema alienda dukani hakumkuta, hivyo aliendelea kumtafuta kwenye vilabu viwili vya pombe ambako hakumkuta.

Mama huyo ameeleza aliamua kurudia nyumbani alikouliza iwapo amerudi lakini jibu likawa hajarejea.

Amesema alitoka tena kwenda kumtafuta na alipokuwa njiani alimsikia balozi akiongea kwa simu huku akitaja jina lake (mama Eliza) kuwa anamtafuta.

“Nikashtuka kwa nini ananitaja, kuna mtu akamwambia mama Eliza unayemtafuta huyu hapa huku akinieleza kuwa natafutwa na balozi. Nikauliza kwani kuna nini? Nikaambiwa kuna mtoto kaokotwa huko ubalozi wa pili,” amesema.

Anaeleza majibu hayo yalimfanya kumweleza naye alikuwa akimtafuta mwanaye aliyeondoka na baba yake.

Mama huyo anaeleza walikubaliana waende wote huko alikookotwa mtoto.

Walipofika anasimulia walimkuta mama akiwa amempakata mtoto.

“Nikamuuliza nani kamleta huku? Mama akanijibu baba yake. Akasema yeye alikuwa amelala lakini Stephen alimgongea mlango, alipotoka akakuta mtoto amewekwa kwenye kizingiti ndiyo maana ameamua kwenda naye kwa balozi,” amesema.

Anaeleza alimhoji iwapo mtoto ni mzima na majibu ya mama yake yalikuwa mwanaye yu mzima.

“Nikamwambia mama naomba nimnyonyeshe, akasema mwache kwanza, utamnyonyesha tu. Tukaenda kituo cha polisi na baadaye tukaja hospitali. Baadaye tuliitwa tena kwenda kutoa maelezo,” anasema.

Anaeleza walitoka kituoni akiwa ameongozana na mama yake, balozi na polisi kwenda kumtafuta mtuhumiwa (mume wake) ambaye hawakumpata.

Anasema baada ya kumkosa kwa rafiki na ndugu zake, polisi walimtaka apumzike nyumbani lakini alikataa akitaka kwenda hospitali kumuona mwanaye.

Anasimulia baada ya kung’ang’ania kwenda kumuona mtoto, waliamua kumweleza ukweli kuwa mtoto amefariki dunia hivyo ajikaze na kuvumilia.

Asia Juma, mjumbe wa kamati ya kitaifa ya kupinga ukatili wa kijinsia, amesema kitendo kilichofanyika hakikubaliki na wataendelea kukipinga.

“Wito kwa jamii, familia na kaya tuwe walinzi wa watoto,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi Septemba 2 alisema mtuhumiwa Damas, mkazi wa Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota mkoani Dodoma anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti hadi kusababisha kifo cha mtoto wake mwenye umri wa miezi sita.

“Jamii iendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwa masuala haya ya ukatili wa kijinsia na watoto ni mtambuka ili kukomesha ukatili huu,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 2, bibi wa marehemu, Elizabeth Sudai alidai mkwe wake (Damas) alifika kwake Septemba mosi saa tatu usiku na kumgongea mlango.

“Nilikuwa nimelala, akaniita, mama, mama mjukuu wako huyo hapo. Nikatoka nikakuta mtoto amelazwa kizingitini. Niangalie aliyemleta mtoto, nikaangaza lakini sikumpata,” alisema.

Alisema alipombeba mtoto hakuwa akitikisika bali amelegea hali iliyomfanya kutafuta majirani akawaeleza kilichotokea.

Baada ya kushauriana na majirani, alisema walikwenda kwa balozi kisha hospitali ilikogundulika kuwa mtoto amefariki dunia baada ya kubakwa na kulawitiwa.

Balozi wa Shina namba tano, katika Mtaa wa Mbuyuni, Tausi Rashid alisema mtoto alipofikishwa kwake, aligundua kuwa hana fahamu, hivyo alipiga simu kwa polisi kata aliyetoa maelekezo waende kituo kikuu cha polisi.

Alisema walikwenda polisi na baadaye hospitali ilikogundulika kuwa mtoto alilawitiwa.

Related Posts