Unguja. Wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji (Babu Duni) akiagwa leo, chama hicho kinaanza utekelezaji wa sera ya ya kuwaenzi viongozi wake wastaafu.
Babu Duni ameachia ngazi mapema mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na Othman Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Sera hiyo inaeleza namna ya kuwaenzi viongozi wa chama hicho waliokitumia kwa heshima, bidii na uaminifu.
Viongozi wanaohusika na sera hiyo moja kwa moja ni kiongozi wa chama mstaafu na mwenyekiti wa chama mstaafu.
Kwa sasa watakaonufaika na sera hiyo ni Juma Duni Haji (mwenyekiti wa chama mstaafu) na Zitto Kabwe (kiongozi wa chama mstaafu).
“Kwa kutambua mchango wao mkubwa katika ujenzi na ustawi wa chama, sera hii inaweka mazingira ya kuhakikisha kuwa viongozi wastaafu wanaendelea kutambulika na kuheshimika na chama na jamii,” inasema sehemu ya sera hiyo.
Hata hivyo, ili viongozi hao wanufaike na sera hiyo lazima wasiwe wamekihama chama au kufukuzwa chama, wakitumikie chama kwa heshima na utii.
Pia, kamati ya uongozi Taifa itakuwa na dhamana ya kuamua iwapo kiongozi husika alikitumikia chama kwa heshima na utii.
Malengo ya sera hiyo ni kuwaenzi viongozi wastaafu, kulinda heshima viongozi, kutambua mchango kuendelea kunufaika na mawazo na fikra za viongozi wastaafu katika ujenzi wa chama, kuwatunza na kuwahudumia viongozi wastaafu kadri ya uwezo wa chama.
Katika kuwaenzi viongozi hao, chama kinahakikisha wanapata gari ambalo aina yake itaamuliwa na kamati ya uongozi wa Taifa, pia wanapata posho ya kila mwezi ambayo kiwango chake pia nacho kitaamuliwa na kamati hiyo.
Manufaa mengine ni kupata bima ya afya na iwapo kiongozi husika atakuwa hana nyumba chama kitamlipa pango la nyumba kwa kiwango kitakachoamuliwa na kamati ya uongozi Taifa.
Mbali na manufaa hayo kamati ya uongozi inaweza kumpatia tuzo maalumu kiongozi huyo kulingana na mchango alioutoa na viongozi hao watashiriki vikao vya maamuzi kulingana na utaratibu utakaowekwa na katiba ya chama.
Viongozi wengine wanaweza kunufaika kwa kadri ya uwezo wa chama.
Pia, chama kinaweza kuwezesha masuala hayo au sehemu kwa vingozi wastaafu makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Zanzibar, Mwanasheria mkuu wa chama.
Wengine ni kiongozi, mtendaji au mwanachama mwingine yeyote mwenye mchango wa kipekee katika kukilinda, kukipigania na kukitetea chama kadri itakavyoamuliwa na kamati ya uongozi.
Akizungumza kuhusu utaratibu huo mchambuzi wa siasa kisiwani hapa, Ussi Ali Ussi amesema ni utaratibu mzuri unaopaswa kuigwa na vyama vingine ili kuwaheshimisha viongozi wao
Hata hivyo, amesema ipo haja sera hiyo kuwatambua viongozi wote wakuu kwani katika mazingira ya kisiasa wote wanafanya kazi kubwa ya kujenga na kumarisha chama
“Hili ni wazo zuri na linapaswa kuigwa na vyama vingine, japo wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kwa baadhi ya vyama kutokana na kutokuwa na mapato ya kujitosheleza,” amesema.