12 watoa ushahidi kesi ya ‘waliotumwa na afande’

Dodoma. Kesi ya jinai ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam inaendelea leo Jumatano Septemba 4, 2024.

Tayari mashahidi 12 wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo inayosikilizwa faragha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Septemba 3, 2024 nje ya Mahakama, wakili anayewawakilisha washtakiwa, Meshack Ngamando alisema jana walisikilizwa mashahidi wawili.

Alisema shahidi mmoja walikamilisha kumhoji maswali ya dodoso na mwingine hakukamilisha ushahidi kutokana na muda kuwa umekwisha.

“Huyu tutaendelea naye kesho (leo)kuanzia saa 6.00 mchana,” alisema Ngamando.

Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa Agosti 19 baada ya washtakiwa kufikishwa mahakamani.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti huyo anayetambulishwa mahakamani kwa jina la XY.

Related Posts