Dodoma. Serikali imeanza mchakato wa kupitia mikataba ya ubinafsishaji wa viwanda vya mazao ili kubaini iwapo ulikidhi masharti.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hayo leo Septemba 4, 2024 alipojibu swali la mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Kungu.
Mbunge huyo amesema moja ya sababu ya kubinafsisha kiwanda cha kubangua korosho cha Tunduru ni kupata mwekezaji anayeweza kukiendesha.
“Serikali haioni kuwa mwekezaji amekosa sifa ya kubinafsishwa kiwanda kile kwa kushindwa kukiendeleza kiwanda hicho,” amehoji Kungu.
Amesema kiwanda hicho kilikuwa kinatoa ajira kwa wanawake 600 na vijana 200, hivyo kuhoji kwa nini Serikali isimlazimishe mwekezaji kukirejesha kiwanda hicho serikalini ili kutafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kukiendeleza na hatimaye wanawake hao waweze kupata ajira.
Waziri Bashe amesema Serikali imeanza mazungumzo na Msajili wa Hazina ili kuona masharti ya ubinafsishaji yalikuwaje.
“Tatizo hili la watu waliobinafsishiwa viwanda lakini kwa wakati huohuo ni wasafirishaji wa malighafi, wengi walichukua viwanda vya korosho na kuvifunga, halafu wakawa wasafirishaji wa korosho ghafi,” amesema.
Amesema tatizo hilo lipo katika korosho na chai, ambako watu walichukua viwanda na mashamba lakini hawajayaendeleza tangu walivyopatiwa.
Amesema Serikali imeanza mchakato wa kupitia mikataba ya ubinafsishaji na kuangalia kama walikidhi masharti wakati wanauziwa viwanda hivyo ili iweze kuchukua hatua.
Katika swali la msingi, Kungu amehoji ni kwa nini kiwanda cha kubangua korosho cha Tunduru kimesimama kufanya kazi kwa miaka saba mfululizo.
Bashe amesema kiwanda hicho kilijengwa na Serikali mwaka 1981.
Amesema kutokana na mabadiliko ya kisera, Serikali ilibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni ya Korosho Afrika Ltd mwaka 2001.
“Kiwanda hicho chenye uwezo wa kubangua wastani wa tani 3,500 kiliendelea na shughuli za ubanguaji hadi msimu wa mwaka 2019/20 kiliposimamisha ubanguaji kutokana na hasara tofauti na matarajio ya mwekezaji,” amesema.
Bashe amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina imeanza kupitia upya hali ya uzalishaji wa viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa kikiwamo kiwanda hicho ili kujadiliana na kuhakikisha wawekezaji waliopo wanafufua viwanda hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa.