WAKATI jana viongozi wa Azam FC wakitangaza kufikia makubaliano ya pande mbili kuachana na Kocha Youssouph Dabo raia wa Senegal sambamba na wasaidizi wake wote aliokuja nao, taarifa zinabainisha kwamba Juma Mgunda anapigiwa hesabu. Na kama wakikubaliana inaelezwa mshahara wake kwa mwezi utakuwa Sh20 milioni.
Dabo aliyedumu ndani ya Azam kwa mwaka mmoja, ameondolewa rasmi jana. Mwanaspoti lilidokeza kuhusu uongozi wa timu hiyo kuzungumza na kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge kama chaguo lao la kwanza na Nasreddine Nabi wa Kaizer Chiefs ambaye taarifa za awali zilieleza alikataa ofa.
Wakati uongozi wa timu hiyo ukiweka tageti kubwa kwa Ibenge, pia Kocha wa Simba Queens, Juma Mgunda naye amewekwa kwenye rada yao kama mbadala.
Chanzo cha ndani kutoka Azam, kinaeleza uongozi umecheki na Mgunda, ingawa bado hawajafikia naye muafaka. Inaelezwa kwamba mkwanja atakaovuta Azam si chini ya Sh20 milioni kutokana na uzoefu wake na posho anazovuta akiwa na Simba kwa sasa na huenda fungu hilo likamueka kileleni mwa makocha wazawa wanaolipwa zaidi nchini. “Ukitaja makocha wazawa wanaolipwa pesa ndefu, Mgunda ni kati yao, uongozi bado unazungumza naye, wakati huohuo tageti kubwa ikiwa ni kumpata Ibenge, hivyo mambo yakikaa sawa lolote linaweza likatokea,” alisema.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Azam, Thabith Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote juu ya benchi la ufundi la timu hiyo, mambo yakikaa sawa wataufahamisha umma.
Kwa upande wa Mgunda akizungumzia ishu ya kuhusishwa na timu nyingine mbali na Simba Queens, amesema ni kweli ofa zimekuwa nyingi lakini hivi sasa sio wakati sahihi kuzungumzia masuala hayo kwani yupo bize kukiandaa kikosi cha Taifa Stars kuelekea mechi za kufuzu Afcon.
Azam jana ilipotangaza kuachana na Dabo na wasaidizi wake, imesema kwa sasa program za mazoezi zitakuwa chini ya makocha wa timu zao za vijana. Nini maoni yako, Mgunda asaini Azam? 0658-376 417