Huyu ndiye Hamza kitasa aliyeiteka Simba SC mapema

UWEZO wa kucheza kulia au kushoto katika eneo la beki wa kati ni miongoni mwa mambo ambayo yanambeba mzawa, Abdulrazack Mohamed Hamza ambaye ameanza kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na kiwango alichokionyesha akiwa na wekundu hao wa Msimbazi katika michezo ya mwanzoni mwa msimu huku akiibua vita mpya.

Hamza ambaye ni ingizo jipya katika dirisha lililopita la usajili, akitokea SuperSport United ya Afrika Kusini hakuwa akipewa nafasi na wengi kabla ya kuanza kuonyesha ubora wake katika mchezo wa mshindi wa tatu kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Nyota huyo wa zamani wa Namungo kabla ya kwenda Afrika Kusini, alipata nafasi ya kuvaa uzi wa wekundu hao wa Msimbazi baada ya Chamou Karaboue ambaye alikuwa akicheza na Che Malone kupata majeraha baada ya mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ambao walipoteza kwa bao 1-0.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alikuwa na majina mawili katika kikosi chake, Hamza na Hussein Kazi (mabeki wa kati) lakini baada ya programu kadhaa za mazoezi iliamua kuanza na nyota huyo ambaye amezaliwa Machi 23, 2003. Hamza kushoto huku Che Malone akiwa kulia katika pacha mpya ya mabeki wa kati tofauti kabisa na ile ambayo ilianza kuonekana katika Tamasha la Simba Day.

Utulivu, uwezo wa kunyang’anya mpira na hesabu za kukabiliana na washambuliaji hasa ana kwa ana (1v1) vimemfanya kuanza kuzungumzwa ndani ya michezo mitatu ambayo ameichezea Simba, miwili ikiwa ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ndani ya michezo hiyo, Simba haijaruhusu bao, ilianza kwa kushika nafasi ya tatu kwenye Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Salehe Karabaka, Hamza na Che Malone walifunga njia za Coastal Union huku pembeni wakicheza Shomary Kapombe/Kelvin Kijili na Mohammed Hussein.

Ubora wake uliendelea kuonekana katika mchezo wa kwanza wa Simba katika ligi wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United kisha akaaminiwa tena dhidi ya Fountain Gate ambapo Mnyama aliendeleza makali yake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0. Ndani ya dakika 270 alizocheza, Hamza kwa kushirikiana na Che Malone kama mabeki pacha wa kati, Simba haijaruhusu bao.

Ni nadra kuona beki anayetumia mguu wa kulia zaidi kucheza eneo la beki wa kati kushoto, hilo ndio eneo ambalo lilikuwa likimpa wakati mgumu msimu uliopita Che Malone wakati huo kulia kwake alikuwa akicheza Henock Inonga Baka ambaye kwa sasa anaichezea AS FAR ya Morocco.

Che Malone ni mzuri akicheza beki wa kati lakini kulia hivyo ni kama Fadlu amemtua mzigo nyota huyo wa zamani wa Coton Sport FC ambao alikuwa nao msimu uliopita, amefanya hivyo akiwa na Chamou na hata Hamza.

Achana na urefu wa 5.9ft alionao ambao unamfanya kuwa na uwezo wa kucheza mipira ya juu lakini pia kasi ni kati ya vitu vinavyombeba ukimtofautisha na Chamou ambaye pamoja na uwezo mzuri aliona anaonekana kuwa mzito hivyo hilo linamfanya kufika kwa haraka katika maeneo muhimu wakati wakishambuliwa.

Hamza sio mchezaji mgeni ligi kuu, ana uzoefu wa kutosha ambao ameupata akiwa na Namungo, KMC na Mbeya City kabla ya kwenda Afrika Kusini.

Licha ya kwamba hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha SuperSport United, lakini kitendo cha kuwa sehemu ya timu hiyo na kushiriki katika michezo kadhaa hata kama ni kukaa benchi ni wazi kuwa kuna mambo ambayo alikuwa akijfunza.

Hapa Hamza anaeleza hilo: “SuperSport United ni miongoni mwa timu kubwa na nashukuru kwa nafasi ambayo nilipata. Nimejifunza mambo mengi kwa sababu nilikutana na wachezaji wenye ubora tofauti tofauti na nilijitahidi kujisukuma kadiri naweza ili kuinua kiwango changu na kupata nafasi ya kucheza.”

Akizungumzia ubora wa mabeki wake wa kati, akiwemo Hamza, Fadlu anaamini kila mmoja atakuwa na nafasi ya kupigania timu hiyo kulingana na wingi wa michezo uliopo mbele yao kuanzia katika mashindano ya ndani hadi kimataifa.

“Msimu huwa na mambo mengi, muda mwingine kuna vitu ambavyo ni ngumu kuvidhibiti mfano majeraha, ni vizuri kuwa na wachezaji wenye ubora wa namna yao ili wakati ambao mmoja anakosekana basi anakuwepo mwingine wa kuendeleza gurudumu, binafsi natamani kuwa nao wote wakiwa fiti,” alisema.

Related Posts