Kwa mujibu wa meya wa mji Lviv, Andriy Sadovyi, watoto watatu walikuwa miongoni mwa waliouawa kwenye mashambulizi hayo, ambayo hadi asubuhi ya Jumatano (Septemba 4) bado yalisababisha mifumo ya anga ya Ukraine kuendelea kuvuma wakati ikiendelea kuzisaka na kuzidunguwa droni kutokea Urusi.
“Hadi muda huu ambapo ni saa mbili asubuhi, zaidi ya watu 35 wanatibiwa. Wengi wao wako kwenye hali mbaya, wakiwemo watoto watano. Tumepoteza watu watatu, akiwemo mfanyakazi wa huduma za afya. Hasara kubwa, zaidi ya majengo 50. Sehemu kubwa ya kiini cha mji wetu, turathi ya kihistoria.” Alisema meya huyo kupitia mtandao wa Telegram.
Soma zaidi: Putin asema uvamizi wa Ukraine Kursk haujawa na athari
Mashambulizi hayo ya Urusi yameharibu pia jengo moja lenye makaazi ya watu katikati ya mji huo karibu sana na kituo kikuu cha treni baada ya jengo hilo kushika moto.
Majengo mawili ya skuli, yaliyo umbali wa kilomita 70 kutoka mpaka wa Poland pia yaliharibiwa. Kutokana na kukatika kwa umeme, shirika la reli lilipaswa kutumia treni zinazotumia dizeli.
Mashambulizi ya Jumatano yalifuatia yale ya jana Jumanne (Septemba 3), ambapo zaidi ya watu 50 waliuawa na wengine 270 walijeruhiwa kwa kombora la Urusi kwenye mji wa katikati mwa Ukraine, Potlava, yakiwa mashambulizi mabaya kabisa kuwahi kufanywa na Urusi ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka miwili ya vita vyake.
Licha ya kwamba Kiev inapatiwa silaha na mataifa ya Magharibi, lakini hali inaonesha kuwa msaada huo haujaweza kubadilisha uhalisia wa kijeshi kwa upande wa Ukraine.
RaisVolodymr Zelensky amekuwa mara kwa mara akiwatolea wito washirika wake kuongeza idadi na viwango vya silaha, yakiwemo makombora ya masafa marefu, ili kuisaidia Ukraine kujilinda kutokana na mashambulizi ya anga ya Urusi.
Urusi yafanyia marekebisho itifaki ya nyuklia
Urusi, kwa upande wake, ilisema siku ya Jumatano kwamba inafanya mabadiliko kwenye itifaki yake ya silaha za nyuklia, ambayo inataja masharti ambayo Urusi inaweza kuzitumia silaha hizo, kutokana na hatua ya mataifa ya Magharibi kuongeza msaada wao kwa Ukraine.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alisema mabadiliko hayo yamechochewa na vitisho vya mataifa ya Magharibi na ameiokosowa Marekani kwa kuharibu makubaliano ya baada ya Vita Baridi barani Ulaya.
Soma zaidi: Putin asifu kasi ya vikosi vyake dhidi ya Ukraine
Peskov alisema mataifa ya Magharibi yalikuwa yamekataa majadiliano na Urusi na badala yake yameamua kufuata njia ya mashambulizi dhidi ya maslahi ya kiusalama ya Moscow, huku ikiitumia Ukraine kama mahala pa kushambulia.
“Ni Marekani ndiyo kinara wa mchakato huu kuchochea hali ya wasiwasi.” Alisema Peskov.
Wizara ya mambo ya kigeni kupitia msemaji wake, Maria Zakharova, ilionya kuwa endapo Urusi itashambuliwa na silaha za masafa marefu, jibu lake litakuwa la haraka na lenye maumivu makali sana.
Vyanzo: AFP, Reuters