Masikini Mdamu bado anataabika, anahitaji msaada

JE, unataka kujua maisha ya aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu yanaendeleaje kwa sasa, Mwanaspoti limefanya mahojiano naye maalum kwa kumtembelea nyumbani kwake Kimara Bonyokwa, Jijini Dar es Salaam ambako  amefunguka mambo mengi.

Kwa mdau au taasisi inayopenda kumsaidia Mdamu kwa fedha, vifaa tiba au matibabu wawasiliane naye mwenyewe kupitia namba yake; 

0655-670101
(itasoma Juliana Malekel)

Ikumbukwe Julai 9, mwaka 2021 basi la timu ya Polisi Tanzania, lilipata ajali likitoka katika mazoezi Uwanja wa TPC Moshi kuelekea kambini, ambapo Mdamu alivunjika miguu yote miwili, jambo ambalo liliwagusa Watanzania wengi kujitoa kwa ajili ya matibabu yake.

Tangu kipindi hicho, kilichobadilika kwa Mdamu anaweza akatembea bila magongo, labda itokee anajisikia vibaya ndio anatumia, lakini bado hajapona. Anaweza kujihudumia kwa maana ya kuoga,kutembea bila kushikiliwa na vitu vingine. “Haikuwa rahisi kufika hapa, japokuwa unaweza ukaona paja langu la kulia linavyovuja usaha ambapo ukizidi nakwenda kusafishwa hospitali na kwa usalama zaidi madaktari wameniambia nisipazipe uchafu niuache uendelee kutoka,” anasema.

Anaendeleaje na timu yake ambayo kwa sasa imeshuka daraja?  “Siku iliyokuwa inashuka daraja tulikuwa tuingiziwe mshahara, haukuwekwa hadi leo, hakuna kinachoendelea tena.”

Kama kuna kitu kinamuumiza na kuitafuna akili ya Mdamu ni kuona majukumu aliyopaswa kuyabeba kama mwanaume, anayafanya mkewe, akisubili kuletewa kila kitu ndani, kwani bado hajaimarika kiafya na anapatiwa huduma ya kwanza kwenye kituo cha afya cha Kigamboni.

Uso wake ukiwa umejaa huzuni na kope za macho yake zikiwa zinalenga machozi wakati akisimulia maisha anayoyapitia kwa sasa.

“Napitia nyakati ngumu, naona giza sijui nuru nitaiona lini, ili niweze kusimama kama mume wa Juliana, watoto Brighton (9) anasoma darasani la tatu, Yully (4) anasoma chekechea,” anasema na kuongeza:

“Mke wangu anafanya kazi ya kuuza chakula katika  mgahawa wa mtu, kwa siku analipwa Sh5,000, hiyo apunguze nauli, tupange bajeti ya chakula na mahitaji ya watoto shuleni.

“Anatoka nyumbani saa 4:00 asubuhi na kurudi saa 3:00 usiku, kuna wakati kazini kwake akiingiza hasara anarejea mikono mitupu, hivyo siku hiyo inakuwa ngumu, kinachokuwa kinaniumiza ni watoto.”

Anaeleza kwamba siku ambayo alijikuta ana kufuru na kulia akiwa amejifungia chumbani, alipokea simu kutoka kwa mkewe akiwa kazini na kumwambia bosi wake amemkata pesa, baada ya hesabu kufeli.

“Siku hiyo aliniambia baba, leo usiku sijui itakuaje, leo sitapewa pesa, bosi kasema nimeingiza hasara, nikaanza kuwapigia marafiki zangu wa karibu wakawa nao hawana pesa, mmoja akanitumia saa 2:00 usiku Sh.5000 ambayo tukanunulia chakula na watoto.

Anaongeza: “Kuna wakati nawaza mfano mke wangu apate changamoto nitaendeshaje familia yangu? pia mke anahitaji matunzo licha ya kunivumilia kwa kipindi kirefu.”

Anasema kuna kipindi anakwenda baa iliyopo jirani na kwake, anakuwa anawaomba washikaji wake asimamie ‘pool table’ ambapo analipwa Sh2000 zinazomsaidia kununua chakula.

“Nikisimama muda mrefu miguu inakuwa inawaka moto, hivyo kuna wakati inanibidi nikae, sasa hakuna mtu ambaye atapenda umfanyie biashara yake kwa kujivutavuta, hivyo washikaji zangu ni kama msaada wananipa,” anasema.

Lipi amejifunza kutoka kwa mkewe? Mdamu anasema kabla ya kupata ajali hiyo alimuonyesha maisha ya uaminifu, jambo linalomfanya aendelee kushikamana naye hadi leo.

“Japokuwa ni binadamu sikuwa malaika, nilijitahidi sana kuwa wazi kwake, kuna wakati akikaa huwa ananiambia Mdamu haya ni matunda ya upendo wako wa kwangu siwezi kukuacha hata tupitie magumu kiasi gani,anaamini tutavuka na nitarudi katika hali yangu ya kawaida ya kujitafutia maisha,” anasema.

Haoni ishu ya kufanya nje na soka, siyo tu kurejea uwanjani, akipata nafasi ya kusomea ukocha atakuwa bado yupo katika ramani ya kuzitimiza ndoto zake.

“Kipaji changu ni soka, endapo nikitibiwa nikipona kabisa, ikishindikana kurejea uwanjani, basi nisomee hata ukocha, kwa sasa ni ngumu kufanya hayo, kutokana na hali duni niliyonayo kiuchumi,” anasema.

Anasema furaha yake katika nafasi yoyote atakayokuwepo katika soka, atatamani kuona vijana wenye ndoto kubwa zinatimia

”Sijui Mungu alichonipangia, ila naamini ipo siku nitaishi kile ninachokiwaza.”

Mdamu anahitaji matibabu zaidi, mguu wake wa kushoto hakanyagii chini, unahitaji kufanyiwa upasuaji eneo la vidole na mapajani, wakati paja la mguu wa kulia linatoa usaha ambao anakuwa anakwenda kuusafisha hospitali.

Anaulizwa ni kiasi gani kinahitajika ili kurudia upasuaji wa mguu wa kushoto? Anajibu, “sijauliza, mara ya mwisho kufanya vipimo (x ray), nilienda kwa nauli ya msaada wa daktari na alinipima bure, hivyo sikuwa na nguvu ya kumuuliza maswali mengi.

“Mguu wa kulia unatoa usaha, hivyo sijui ndani kuna nini, ingawa madaktari wananiambia bora unavyotoka nje, kuliko kubakia ndani, hivyo nakatazwa kuziba.” Anasema alipofikia ni neema ya Mungu na Watanzania waliojitoa usiku na mchana, kupigania uhai wake, anawaomba wasimchoke, anahitaji msaada wao, ili aweze kutibiwa na kufanya majukumu mengine.

“Hadi nilipofika namshukuru Mungu, natembea japokuwa siyo kwa umbali  mrefu, ninachotamani ni kupona kabisa ndipo nitapata nguvu ya kuanza kupambana kujitafutia mwenyewe, ila kwa sasa imekuwa ngumu. Nikitembea sana miguu inawaka moto.”

“Afya ni kila kitu katika mwili wa binadamu, kuna wakati akili inawaza hata nikafanye vibarua nipate chochote kitu, lakini nashindwa.”

Anasema baada ya jina lake kuanza kujulikana kupitia kipaji chake cha soka , alishangaa anatafutwa na ndugu zake waliokutana kwa baba yake (mzee Mdamu).

“Mama yangu alishafariki muda mrefu tukiwa wadogo, tumezaliwa kaka mkubwa aliyekuwa ananiuguza Benedicto, dada Rebecca na mimi, nje na familia yake ya sasa baba yangu sikuwahi kujua ana watoto wengine ambao hata yeye hakuwa anawasiliana nao.”

“Baba nimemuunganisha na watoto wake wanafika sita, walinipigia simu kila mmoja kwa wakati wake ananiuliza unajiita Gerald Mathias Mdamu tueleweshe vizuri kuhusu huyo mzee, baadaye wakagundua ni baba yao walikuwa wanamtafuta, hapo ni kutoka mama tofauti.

“Kali zaidi nikakutana na mchezaji mwenzangu Athanas Mdamu ambaye amecheza (2013-2018) Alliance Academy, (2018) Singida United, (2019) Kariobangi Sharks ya Kenya na (2019) Alliance Academy, katika kuulizana nikagundua ni mtoto wa mzee.”

Anapoulizwa msaada wa ndugu zake upoje kwake? Anajibu: “Ni dada yetu mmoja ndiye mwenye afadhali, akiwa anataka kunisaidia anakuwa anakumbwa na changamoto kila kitu kinavurugika, kuhusu mzee kashazeeka anahitaji msaada wa watoto wake, hivyo ndivyo mambo yalivyo.”

PACOME, AZIZ KI, AHOUA, FEI TOTO

 Anasema anafuatilia kinachoendelea Ligi Kuu Bara, licha ya kuwa nje ya kazi, anavutiwa zaidi na baadhi ya wachezaji kama Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki (Yanga), Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Azam FC), kuhusu Simba anaona kuna wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa ila bado hawajaanza kuonyesha kama Jean Charles Ahoua.

“Napenda anachofanya Fei Toto, kiwango chake kinazidi kukua kila msimu, lakini kuna wachezaji wa kigeni wanaofanya makubwa wamekuwa chachu kwa wazawa, ingawa kwangu mimi aliyekuwa mshambuliaji besti (bora)  ni Fiston Mayele alikuwa Yanga na sasa yupo Pyramid ya Misri, msimu anaong’aa zaidi ndio nilikuwa nimeumia,” anasema. 

Kwa mdau au taasisi inayopenda kumsaidia Mdamu kwa fedha, vifaa tiba au matibabu wawasiliane naye mwenyewe kupitia namba yake; 

0655-670101
(itasoma Juliana Malekel)

Related Posts