Watoto wanavyogeuzwa vitega uchumi vya familia Katavi

Katavi. Wakati Serikali inajitahidi kuandaa mazingira na mipango madhubuti ya makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali hali ni tofauti wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi.

Watoto wengi wamekuwa wakitegemewa na familia kwa kufanya kazi ya kuuza matunda na mbogamboga mitaani, badala ya kwenda shuleni.

Hali hiyo imeelezwa kuchochea mimba za utotoni.

Ukipita katika Manispaa ya Mpanda kila asubuhi, ni jambo la kawaida kukutana na watoto wa kike na kiume wakiwa na ndoo zilizojaa vitumbua na maandazi na chupa za chai, wakitembeza mitaani kutafuta wateja.

Baadaye mchana, watoto hao utawakuta wamebeba vikapu vilivyojaa matunda, mbogamboga, ndizi mbichi, mihogo na mayai wakisaka wanunuzi huku wazazi wao wakisubiri kipato kitakachotokana na mauzo hayo.

Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha mimba 13,469 ziliripotiwa kwa watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 19 katika Mkoa wa Katavi, umri ambao watoto hao walitakiwa kuwa shuleni.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Septemba 4, 2024 kususiana na hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Katavi, Kiame John amekiri kuwepo kwa tatizo hilo.

Amesema tayari Serikali ya mkoa imeweka utaratibu wa kufanya doria za mara kwa mara mitaani inayolenga kuwakamata watoto wanaofanya biashara wakati wa masomo.

Amesema doria hiyo imepunguza kwa kiasi fulani tatizo hilo.

John amesema wazazi na walezi wengi wanawatumia watoto katika biashara hizo kwa imani kwamba wanavutia wateja zaidi, jambo ambalo sio sahihi.

“Tunaendelea kufanya doria na kutoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa kupeleka watoto shule badala ya kuwafanya wachuuzi mitaani,” amesema John.

Aidha, amesema Serikali imeanzisha mpango wa makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 8, ambao unalenga kumjengea mtoto misingi imara ya maadili na tabia njema.

Amesema mkakati huo tayari umeanza kutekelezwa mkoani Katavi.

Aisha Maulid, mkazi wa Nsimulwa, Manispaa ya Mpanda, amesema ajira za watoto zinasababishwa na wazazi, hususan kinamama.

Amesema wengi wao huwatumia watoto kama kitega uchumi kwa kisingizio cha kupata fedha kwa ajili ya mahitaji ya shule.

Hata hivyo, mtoto Rebecca Gerald (12) anayefanya biashara ya kutembeza matunda mitaani, amesema: “Mimi nasoma darasa la sita Shule ya Msingi Azimio. Mama huwa ananiandalia ndizi, maparachichi na matango kwenye beseni ili niende kuuza ili tupate pesa ya chakula na mahitaji mengine ya kwangu ya shule.”

Mtoto mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John William (14), amesema aliacha shule akiwa darasa la pili na kuanza kufanya biashara ya kutembeza mbogamboga kwa sababu ya mazingira magumu ya nyumbani kwao.

Lakini mtoto huyo anaiomba Serikali kutoa msaada kwa watoto wa familia masikini nao watimize ndoto zao.

“Naomba Serikali itusaidie kwa mahitaji ya shule na chakula ili na sisi watoto wa masikini tuweze kufikia malengo yetu, sisi hatuna tofauti na watoto wa matajiri isipokuwa ni mazingira tu yanatukwamisha,” amesema John.

Mkazi wa manispaa hiyo, Kelvin Simpasa amesema tatizo la ajira za watoto katika Manispaa ya Mpanda ni kubwa.

Amesema kama Serikali haitalivalia njuga, itaendelea kuathiri maisha ya watoto wengi.

“Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha watoto hawa wanapata fursa ya kwenda kusoma badala ya kujikita kwenye biashara hii inayowaathiri hata kwenye ukuaji wao,” amesema mkazi huyo.

Related Posts