Dar es Salaam. Wakati zabuni za zaidi ya Sh840 bilioni za urejeshaji miundombinu iliyoharibiwa na mvua zikitarajiwa kutangazwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), makandarasi ‘makanjanja’ wamekalia kuti kavu.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameziagiza Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuanza kushughulika na kampuni zinazopewa kazi na wateja, taasisi za Serikali na binafsi lakini haziwajibiki katika usimamizi wa ujenzi.
Bashungwa amesema hayo leo Jumatano Septemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam, alipofungua mkutano kuhusu masuala ya ujenzi uliowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wahandisi na makandarasi.
Bashungwa amesema kati ya wiki hii na wiki ijayo, zabuni hizo zitaanza kutangazwa, kipaumbele kikiwa kwa wakandarasi wazawa.
“Sisi kazi yetu tutasimamia fedha hizi, dhamira kubwa na kipaumbele ni kuwawezesha makandarasi wazawa kushiriki katika ujenzi wa miundombinu hii,” amesema.
Hata hivyo, amewataka makandarasi kusimamia na kuheshimu misingi ya taalamu yao pindi wanapopewa kazi, kwani amekuwa akipokea malalamiko juu ya utekelezaji duni wa ujenzi wa majengo yanayojengwa na makandarasi wa ndani.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuwezesha makandarasi wazawa, jambo lililofanya baadhi ya masharti kuboreshwa ili kutoa fursa kwao.
“Naomba sana kabla hatujawachukulia hatua mjirekebishe, hasa wale makandarasi mnaochukua tenda za majengo. Mnaposaini tu mkataba, uswahili unaanza hadi mteja anajiuliza kuwa hawa ndio wazawa ambao Serikali inawatengenezea uwanja kuongeza fursa za kupata kazi,” amesema.
Waziri amesema ipo miradi katika mikoa mbalimbali ambayo wakandarasi wamepewa kazi, ila wateja wanapata changamoto kwa sababu ya uswahili, licha ya kupewa malipo ya awali.
“Badala ya kupeleka malipo hayo katika ujenzi wa jengo, anapeleka kwenye matumizi mengine. Naomba nianze kuona hatua zinachukuliwa kwa makandarasi kwenye eneo la ujenzi wa majengo ambako makanjanja wanafanya kazi,” amesema.
Amewataka wanaofanya vizuri kutokubali kuharibiwa sifa na wachache wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amezitaka ERB na CRB kushirikiana kwa karibu kushughulika na wachache wanaoharibu heshima ya taaluma ya uhandisi.
“Nimeiagiza CRB na ERB kama sheria ni dhaifu, basi ziletwe wizarani zipelekwe bungeni ili kuhakikisha dhamira ya kusaidia wahandisi na wasanifu majengo wa ndani kwa kupata mazingira wezeshi inazaa matunda,” amesema.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Chemba ya Sekta ya Ujenzi na Miundombinu Tanzania (CCIT), Steven Mkomwa amesema watahakikisha wanawasimamia walio chini yao wafuate misingi inayotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Wakati Waziri Bashungwa akisema hayo, Agosti 30, 2024 mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko aliomba mwongozo wa Spika bungeni akitaka makandarasi wa ndani kulipwa kwa wakati au kulipwa riba pale malipo yao yanapochelewa kama ilivyo kwa wale wa kigeni.
Matiko akitumia kanuni ya 76 kuomba mwongozo wa Spika kuhusu utata wa majibu ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipojibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Bupe Mwakang’ata.
Mbunge Mwakang’ata aliuliza swali la nyongeza kwenye swali la msingi lililoulizwa na mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso kuhusu malipo ya makandarasi wazawa.
Mwakang’ata alitaka kujua ni kwa nini makandarasi wa nje wanapocheleweshewa malipo hulipwa na riba, lakini wa ndani wanapocheleweshwa hawalipwi riba.
Matiko alisema wabunge wamekuwa wakipokea malalamiko mengi ya makandarasi wa ndani ya kutolipwa kwa wakati, baadhi inapita miaka mitano na hata saba bila kulipwa.
“Makandarasi wa ndani unakuta wamekopa fedha na wakati mwingine wanatelekeza kazi au wanafanya kazi zao kwa kiwango cha chini. Nimesimama kuomba mwongozo wako, makandarasi wa ndani lazima tuwatie moyo, tumewasomesha na wanavyopata kazi na kulipwa kwa wakati ndiyo wanavyopata ujuzi zaidi,’ alisema Matiko.
Dk Mwigulu akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa, alisema Serikali haipingi hoja ya Matiko.
“Bunge lililopita Serikali tulileta marekebisho ya sheria ili kuwabeba makandarasi wazawa. Na haya yalikuwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunajenga uchumi wetu kwa kuwawezesha wakandarasi wazawa.
“Kwa hiyo, alichosema mbunge na ambacho Bunge linataka ndicho na sisi Serikali tunachosisitiza. Kwa hiyo, rai yangu kwa makandarasi wenyewe Watanzania wajiamini. Kwa mfano, tuna mikataba ambayo ni kati ya mkandarasi na Serikali, na tuna mikataba ambayo ni ya mkandarasi mzawa na mkandarasi wa nje,” alisema.
Dk Mwigulu alisema hutokea makandarasi wazawa huingia mikataba na wa nje na hawaweki ukomo, na Serikali inapowalipa wa nje kwa Dola wao huchelewa kuwalipa wazawa.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.