CCM yajitenga kauli ya aliyekuwa DC Longido

Arusha. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejitenga na kauli ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido (DC) mkoani Arusha, Marco Ng’umbi kikisema hakihitaji kubebwa ili kishinde katika chaguzi mbalimbali ukiwemo wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Septemba 1, 2024 kulisambaa kipande cha video mitandaoni inayomwonyesha Ngu’mbi akizungumza mambo kadhaa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2020.

Katika picha hiyo jongefu ya dakika 1.32, Ng’umbi anasikika akiwaeleza watu aliowataja mara kadhaa kuwa ni madiwani kwamba ushindi wao katika uchaguzi huo si ujanja wao, bali ni nguvu ya Serikali.

Alikwenda mbali zaidi na kueleza hata waliopita bila kupingwa ni kazi iliyofanywa na Serikali na sio ubora wa wagombea husika.

“Kama kuna mtu ambaye si mwoga ni mimi, wote hapa madiwani mwaka 2020 hayupo diwani aliyepiga kampeni hapa. Sasa yale mazingira ya mwaka 2020 si kwamba yalikuja yenyewe moja kwa moja kwa sababu ninyi mlikuwa wagombea bora sana.”

“Ni mazingira ambayo yalikuwa yametengenezwa na Serikali na Serikali ndiyo iliyoifanya kazi ile ya wewe kupita bila kupingwa. Kuna watu unafahamu kilichotokea huko kwenye pori anasema mimi sijui na mimi nilihusika kwenye majimbo fulani fulani,” alisikika katika kipande hicho cha video.

Jioni ya siku hiyohiyo, kupitia taarifa iliyotiwa saini na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wake na Septemba 2, 2024 alimteua Salum Kali kuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido. Kabla ya uteuzi huo, Kali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma.

Lakini leo Jumatano Septemba 4, 2024 akizungumza na viongozi wa CCM na Serikali wa Mkoa wa Arusha katika kikao cha ndani, Makalla amesema CCM haiwezi kubebwa na hakitegemei mbeleko katika chaguzi, akisema wanakwenda kinyume na kauli ya Ngu’mbi kuhusu uchaguzi.

“Alisema sijui machakani, mi nasema yule aliishiwa hotuba, akaanza kutafuta maneno yake siye (CCM) hayatuhusu na hizo ni habari zake, yaani ilikuwa mazungumzo badala ya habari.”

“Hotuba ilimuishia aliyozungumza hayahusiani na CCM, ndiyo maana tunawataka viongozi wapangilie hotuba zao kwa kuandika vizuri siyo kutengeneza sinema, eti ulikwenda maporini kufanya nini? amesema na kuhoji Makalla.

Makalla amesema CCM haiwezi kwenda porini bali Ngu’mbi alikwenda peke yake iwe kuchimba dawa au kufanya shughuli nyingine.

“Mimi ndiyo msemaji wa CCM, tunawahakikishia Watanzania, chama hiki kimejiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani na tutashinda, hatuwezi kwenda porini kuzurura kwa sababu tuna muundo mzuri kuanzia ngazi ya kata na tuna Ilani nzuri, hatuhitaji mbeleko,” amesema Makalla.

Mwenezi huyo, ameanza ziara ya kikazi ya siku sita katika mikoa ya Arusha na Manyara akisema ina lengo la kutembelea wilaya ambazo hazikufikiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi.

Awali, Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Loi Thomas Ole Sabaya amesema chama hicho kipo pamoja na Serikali katika kufanikisha shughuli za maendeleo.

“Tumekubaliana katika mkoa huu kufanya kazi ya kutatua kero za wananchi tunakwenda kata kwa kata, kwa ushirikiano wa Serikali, tunataka kuhakikisha CCM inashinda tena kwa kishindo,” amesema Ole Sabaya.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo amesema Serikali inafanya kazi mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu hasa barabara za ndani, vituo vya afya na shule mpya za msingi na sekondari ili kurahisisha huduma za elimu.

“Changamoto zilizopo mbugani ni barabara hazipitiki, tunakuomba mwenezi uwahimize wizara ya maliasili zile bajeti tulizopitisha basi zitekelezwe,” amesema Gambo,

Related Posts