WALEED Nahdi ni ingizo jipya la madereva wanaotarajiwa kushiriki raundi ya pili ya mbio za magari ubingwa wa taifa zitakazofanyika Iringa mwishoni mwa wiki ijayo.
Nahdi anakuwa dereva wa 13 kuthibitisha ushiriki wake katika vita hiyo ambayo itafanyika Septemba 14 na 15.
“Ni mtihani mkubwa kwangu, lakini nina imani ya kufanya vizuri kama kijana mwenye ari na uwezo mkubwa wa kuendesha gari kwa kuzingatia kanuni za usalama,” alisema Nahdi ambaye anatoka mkoani Morogoro.
Katibu wa Klabu ya Mbio za Magari ya Iringa (IMSC), Maneno Robert pia alithibitisha kuwepo Nahdi katika orodha ya washiriki wa mbio hizo akiendesha gari aina ya Subaru Impreza N10.
Kwa mujibu wa Robert, nguvu kubwa ya Nahdi iko kwa msoma ramani wake, Awadh Bafadhili kutoka Tanga ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miongo miwili.
“Naamini Bafadhil ambaye ameshiriki mashinbdano mengi ya mbio za magari ndani na nje ya nchi atakuwa msaada mkubwa kwangu,” alisema Nahdi.
“Sitawaangusha wakazi wa Morogoro pamoja na mdhamini wangu Afroil, kwani ndiyo walionipa moyo wa kushiriki.”
Nahdi na msoma ramani wake watakuwa na kibarua dhidi ya bingwa mtetezi Yassin Yasser na msoma ramani wake Ally Katumba kwani wana uzoefu mkubwa kama washiriki wa mbio za magari ya ubingwa wa Africa (African Rally Championship) ambayo huchezwa katika nchi nane za Kiafrika.
Iringa inaandaa raundi ya pili ya ubingwa wa mbio za magari wa taifa (NRC) baada ya Tanga kufungua msimu kwa mbio za kilomita 155, Julai, mwaka huu.
Vilevile atakuwa akikabiliana na madereva wazoefu kama Randeep Birdi wa Dar es Salaam na Gurpal Sandhu wa Arusha ambao walichukua nafazi mbili za juu katika mbio za Tanga. Mbio za magari za Iringa zitaanzia katika Uwanja wa Samora katikati ya mji wa Iringa ambako kutafanyika mbio fupi za Super Special Stage, Jumamosi na kumalizia siku inayofuata, Septemba 15.