Kyiv Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba (43) ametangaza kujiuzulu leo Septemba 4, 2024, ikiwa ni siku moja tangu mawaziri watano walipojiuzulu jana, huku ikielezwa Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskiy anatarajiwa kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.
Kujiuzulu kwa mawaziri hao kunakuja wakati Russia ikiendeleza mashambulizi katika nchi hiyo katika vita kati ya nchi hizo mbili vilivyoanza tangu Februari 24, 2022.
Kwa mujibu wa mashirika ya habari ya kimataifa ya Reuters na Al Jazeera, barua ya kujiuzulu kwa Kuleba imechapishwa kwenye Facebook na Spika wa Bunge la nchi hiyo, Ruslan Stefanchuk, huku Spika akisema hivi karibuni wabunge watajadili ombi hilo.
Bunge linatarajia kupigia kura kujiuzulu kwa mawaziri hao leo Jumatano katika kile ambacho kawaida ni utaratibu wa kisiasa.
Kuleba amekuwa kiungo muhimu katika masuala ya kidiplomasia ya Ukraine na imeelezwa kuwa ofisa wa ngazi ya juu zaidi katika Serikali ya Zelensky kuachia ngazi
Rais Zelenskiy amesema mabadiliko kwa Serikali ambayo yanakuja katika wakati muhimu kwenye mzozo kamili, ni muhimu kuuimarisha na kufikia matokeo yanayohitajika na Ukraine.
“Msimu wa vuli utakuwa muhimu sana kwa Ukraine. Na taasisi zetu za Serikali zinapaswa kusaidiwa ili Ukraine ifikie matokeo yote tunayohitaji kwa ajili yetu sote,” amesema Jumanne.
Wakati huohuo, vikosi vya Russia vinasonga mbele mashariki mwa Ukraine, wanajeshi wa Ukraine wamevamia eneo la Kursk nchini Russia huku Moscow ikizidisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora katika wiki za hivi karibuni.
David Arakhamia, mbunge mkuu wa Chama cha Zelenskiy, amesema kutakuwa na urekebishaji mkubwa wa Serikali na zaidi ya nusu ya mawaziri watabadilika.
“Kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Nje kulikuja wakati takriban watu saba waliuawa na 35 kujeruhiwa katika shambulizi la usiku mmoja huko Lviv,” amesema meya Andrii Sadovyi.
Ukraine imesema moja ya mashambulizi mabaya zaidi ya Russia tangu vita kuanza ni shambulio lililotokea huko Poltava na kusababisha vifo vya watu 50 na kujeruhi wengine 200.