TZ Open kuileta Afrika Arachuga

CHAMA cha Gofu kwa Wanawake Tanzania (TLGU) kimesema kinatarajia kuona nchi nyingi zaidi ya Kenya na Uganda katika mashindano ya mwaka huu ya Tanzania Ladies Open yanayoanza kupigwa jijini Arusha.

Katibu wa Mashindano wa TLGU, Rehema Athumani ameliambia Mwanaspoti kuwa nchi zaidi zitatuma washiriki kwa sababu barua za mialiko zimesambazwa katika karibu nchi zote za Ukanda wa Afrika.

“Mialiko imetumwa kwa vyama na vikundi vyote vya gofu ya wanawake barani Afrika na tunatrajia kuanza kupata majibu kabla ya mwisho wa juma hili,”  alisema katibu huyo wa mashindano.

Kwa mujibu wa TLGU, nchi za Kenya na Uganda zimekuwa zikituma washiriki mara kwa mara katika mashindano mengi ya Tanzania Ladies Open, lakini mwaka huu kuna tegemeo kubwa kuwa nchi zaidi zitatuma washiriki jijini Arusha.

Mashindano ya wazi ya wanawake yanakuja jijini Arusha baada Watanzania kufanya vizuri katika mashindano ya wazi ya wanawake katika nchi za Zambia, Kenya na Uganda mwaka huu.

Madina Iddi, nyota kutoka Arusha Gymkhana Club amekuwa ndiye kinara wa mafanikio hayo baada ya kushinda mataji matatu ya ubingwa wa gofu ya wanawake katika nchi za Zambia na Uganda.

Vilevile kutoka Klabu ya Arusha Gymkhana, Neema Olomi alimefanya vizuri nchini Kenya na Uganda pamoja na Aalaa Somji aliyecheza vizuri katika mashindano ya Zambia na Uganda.

Yakijulikana kama Tanzania Ladies Open, hayo ni mashindano ya gofu ya siku tatu ambayo yatapigwa katika mashimo 54  ya viwanja vya gofu vya Arusha Gymkhana kuanzia Septemba 13 hadi 15 mwaka huu, kwa mujibu wa TLGU.

Mashindano ya mwaka huu yatakuwa ni mtihani mzuri kwa wachezaji wa Tanzania ambao hivi karibuni walifanya vizuri katika mashindano ya wazi ya wanawake nchini Kenya, Uganda na Zambia  kwani yatawapa nafasi ya kuthibitisha tena ubora.

Licha ya Madina aliyeshinda mataji matatu, wachezaji wengine kama Hawa Wanyeche, Neema Olomi, Vicky Elias na Aalaa Riyaz Somji pia waling’ara katika michuano ya hivi karibuni iliyofanyika nchini Kenya na Uganda.

Chipukizi Aalaa Somji pia aling’ara kwa kupiga hole-in-One(ace) licha ya kumaliza katika nafasi ya nne wakati Hawa Wanyeche alimaliza wa pili na Olomi wa tatu katika mashindano ya hivi karibuni ya John Walker Uganda Open.

Katika mashindano ya mwaka huu, yanatarajiwa kuwa na ushindani.

Related Posts