Serikali kuwashika mkono wahasibu wanawake

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuwa mshirika wa kimkakati kuboresha mazingira ya kazi, fursa sawa za maendeleo kwa wanawake wahasibu ili kuandaa viongozi bora wanaotokana na wanawake.

Hayo yamo kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah katika uzinduzi wa kongamano la saba la Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) leo Septemba 4, 2024.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika elimu, mafunzo na kuondoa vikwazo dhidi ya wanawake ili kufikia ndoto zao za kiuongozi.

Amesema endapo wahasibu watatumia nguvu zilizomo ndani yao kikamilifu, watawezesha kufikia malengo ya chama hicho kwa ufanisi.

Rais Samia amesema kongamano hilo ni chachu ya kukumbushana kuhusu thamani ya uwezo wa asili wa mwanamke, jambo ambalo litawawezesha kukabiliana na mazingira yanayowazunguka na kuleta maendeleo chanya na endelevu katika maisha na jamii kwa ujumla.

Amesema uzoefu unaonyesha maendeleo ya kweli na endelevu yanapatikana endapo sauti na mchango wa wanawake vinapewa uzito unaostahili kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Hivyo, amewataka kulitumia kongamano hilo kwa kujenga mtandao imara wa kusaidiana na kuhamasishana kuelekea malengo ya pamoja.

Mwenyekiti wa chama hicho, Dk Neema Kiure amesema mbali ya kuhamasisha wanawake kujiunga katika fani ya uhasibu, pia kimekuwa na kazi mtambuka ya kuhudumia jamii kuhusu masuala ya jinsia, kutoa ushauri wa kitaalamu wa stadi za maisha na ujasiriamali.

Amesema wamewafikia wajasiriamali wadogo-wadogo hasa makundi maalumu kuwafundisha matumizi bora ya mikopo wanayopewa na Serikali ili kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika kupitia mradi wa ‘Bado naweza.’

“TAWCA imewapatia mafunzo wasichana 101 waliopata mimba za utotoni, na wengi wao wamefanikiwa kujiwezesha kiuchumi kwa kuanzisha na kuendeleza biashara binafsi,” amesema. 

Amesema chama hicho kina mpango wa kushirikiana na Serikali katika kupunguza umasikini.

Dk Kiure amesema wamewaunganisha wahasibu zaidi ya 1,000 kushiriki katika harakati za kumkoomboa mwanamke kielimu na kiuchumi nchini.

Amesema makongamano kama hayo husaidia kuimarisha maendeleo ya uongozi, kukuza usawa wa kijinsia, na kuwawezesha wanawake kujiamini kushindana na vikwazo vya maendeleo.

Mkurugenzi mtendaji wa chama hicho, Tumaini Laurance amesema kongamano hilo ni la saba kufanyika tangu kuasisiwa mwaka 2018.

Baadhi ya mafanikio ya makongamano hayo amesema ni kuongeza idadi ya wahasibu wanawake nchini. Amesema mwaka 2015 walikuwa asilimia 23 na mwaka huu, 2024 wamefikia asilimia 37 hali inayoonyesha mwamko wa wasichana kusoma masomo ya hesabu na biashara.

“Ongezeko la wahasibu wanawake limechangiwa na kuondoa dhana ya wanafunzi kutopenda kusoma hesabu. Chama kinaendelea kuhamasisha wasichana kusoma hesabu na masomo ya biashara ili kuongeza namba ya wahasibu wanawake nchini,” amesema.

Kongamano hilo lililobeba kaulimbiu ‘nguvu iliyo ndani yako’ limewashirikisha takribani wanawake 400 wa fani mbalimbali, wakiwamo wahasibu, wakaguzi wa hesabu, rasilimali watu na utawala.

Chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2015 kwa lengo la kuhamasisha wanawake kujiunga kwenye fani ya uhasibu kilianza na wahasibu 18 na sasa kina wanachama 1,011.

Related Posts