Tunduma. Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetumia Sh1.3 bilioni kujenga Shule ya Msingi Kokoto kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za Msingi Katete na Kigamboni, zilizopo Kata ya Mpemba zenye jumla ya wanafunzi 3,500.
Shule hiyo imezinduliwa leo Jumatano, Septemba 4, 2024, na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mzava akisemja itasaidia kupunguza changamoto kwa wanafunzi wa shule hizo mbili.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Casta Mbalawa amesema fedha zilizotumika kujenga jengo hilo, Sh400 milioni zimetolewa na Serikali kuu, Sh500,000 nguvu za wananchi na Sh973.7 milioni zimetokana na mapato ya ndani.
Mbalawa amebainisha kuwa shule za Msingi Katete na Kigamboni zina jumla ya wanafunzi 3,500, huku Shule ya Katete pekee ikiwa na wanafunzi 2,040 na Kigamboni ina wanafunzi 1,460, hali inayosababisha msongamano kwenye vyumba vya madarasa.
Amesema ujenzi wa majengo ya shule hiyo umehusisha vyumba 10 vya madarasa, ofisi nne za walimu, matundu 24 ya vyoo, jengo la utawala na nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa kukaliwa na familia mbili mbili.
“Ujenzi ulianza Januari 2022 na ulitarajiwa kukamilika Januari 2024 kwa ajili ya kupokea wanafunzi, lakini ulisuasua kutokana na upatikanaji wa fedha kwa awamu kutoka kwenye mapato ya ndani. Hivyo, tunaomba wananchi washirikiane kulinda miundombinu ya shule hii sasa,” amesema Mbalawa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mzava, amepongeza juhudi za halmashauri na Serikali kuu kwa kushirikiana katika ujenzi wa shule hiyo.
Amesema kuendelea kujenga madarasa na shule lengo la Serikali inataka kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za umma.
“Niwapongeze sana watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa kutumia mapato ya ndani, Sh973.7 milioni, kujenga shule hii ya ghorofa ambayo ni ya mfano,” amesema Mzava.
Joshua Mwashila, mmoja wa wakazi wa Kata ya Mpemba amesema ujenzi wa shule hiyo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule za Msingi Katete na Kigamboni na kuboresha uwiano rafiki darasani katika shule mpya ya Kokoto.