Pengine unaweza kusema hakuna ofisi nyingine inayojihusisha na masuala ya kisiasa duniani ambayo inahitaji fungu kubwa la fedha, ili kushinda siasa zake kama ile ya mgombea urais Marekani. Hebu turejee nyuma katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2020.
Rais wa wakati huo Donald Trump na mpinzani wake, Joe Biden, walitumia dola bilioni 5.7 sawa na yuro bilioni 5.2 ili kuwashawishi wapiga kura, hii ni kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia ufadhili wa kampeni na ushawishi nchini Marekani.
Katika kampeni za urais mwaka huu zinaonekana kwenda sanjari linapokuja suala la fedha huku Makamu wa Rais ambae pia ni mgombea wa Chama cha Democratic, Kamala Harris, akijipiga kifua kukusanya kiasi cha michango yenye thamani ya dola milioni 310 katika mwezi wa Julai pekee.
Katika upande mwingine wa sarafu kwenye kipindi kama hicho mgombea wa Chama cha Republican na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, alidai kupokea takriban dola milioni 138 za michango.
Kiasi kikubwa cha fedha kinakusanywa sio tu kutoka kwa wafadhili wadowadogo wasio hesabika kadhalika kinatoka kwa matajiri wakubwa na washirika kindakindaki wa Marekani.
Nini huwa nyuma ya wachangiaji vigogo kwa kampeni za wagombea urais Marekani?
Ni ukweli dhahiri kwamba wale wanaochangia mara nyingi zaidi kwenye kampeni za uchaguzi wanatumia mwanya huo kufanikisha harakati zao hapo baadae kupitia michango hiyo.
Kwa mfano Mwanzilishi mwenza wa mtandao wa LinkedIn na mjumbe wa bodi ya Microsoft, Reid Hoffman, alitoa mchango wa kiasi cha dola milioni 7 katika kampeni za chama cha Democratic.
Akizungumza na kituo cha habari cha CNN alisema kwamba hafurahishwi na Mkuu wa Tume ya Biashara Marekani, Lina Khan, ambaye alikuwa “anapiga vita dhidi ya biashara yake Marekani.” Alionyesha wazi matumaini yake kwamba Harris atakapochukua hatamu “atafikiria tena juu ya nafasi hiyo.”
Wakati huo huo, Trump naye amepokea uungwaji mkono wa kisiasa na kifedha kutoka kwa wafadhili wakubwa, akiwemo Timothy Mellon, msaidizi wa Benki ya Pittsburgh, ambaye ameweka kiasi cha dola milioni 50, wengine wanaomuunga mkono mwanasiasa huyo ni Mwekezaji wa teknolojia David Sacks na Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla, Elon Musk.
Soma pia: Uchaguzi wa Marekani: Rais Joe Biden ampisha Kamala Harris
Washirika wa karibu wa Musk wameunda kile walichokiita Super Political Action Committees ama ” super PAC” ili kumuunga mkono Trump, ambayo inatarajiwa kuingiza mamilioni ya dola katika kampeni za kusaka kuchaguliwa tena kwa Trump.
Hakuna michango ya Musk kupitia jukwaa hilo ambayo imeweka wazi kwa Tume ya uchaguzi hadi sasa lakini wandani wa bilionea huyo wanasema anatarajiwa kuunga mkono juhudi.
Wamarekani wanataka ukomo wa michango ya mabwenyenye kwa wagombea urais
Kamati hiyo inahusisha mashirika huru ya kisiasa ambayo wachangiaji wanaweza kutoa kiasi cha fedha kisicho na ukomo. Mnamo 2010, Mahakama ya Juu ya Marekani ilitoa uamuzi ambao umekuwa alama katika mamlaka ya ufadhili wa kampeni.
Uamuzi wa mahakama ulimaanisha kwamba kizuizi chochote cha ufadhili wa kampeni za kisiasa ni udhibiti, unaokwenda kinyume na sheria.
Jörg Hebenstreit, mtaalamu wa siasa za ndani Marekani katika Chuo Kikuu cha Jena nchini Ujerumani, anasema uamuzi huo wa mahakama ni hatua ya mabadiliko katika siasa za Marekani.
Hata hivyo kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew chenye makao yake makuu mjini Washington, watu wazima 7 kati ya 10 wa Marekani wanataka kikomo cha watu binafsi au mashirika kuchangia kwenye kampeni za kisiasa.
Watu wanane kati ya 10 waliohojiwa wanaamini kwamba watu wanaotoa fedha kwenye kampeni za kisiasa wana ushawishi mkubwa kwenye Bunge la Marekani.