Bibi asimulia mjukuu alivyokosa matibabu kisa Sh20,000

Mwanza. Mwamvua Said (75), mkazi wa Kayenze Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza amewezeshwa bure kadi ya bima ya afya kwa ajili yake na wajukuu zake watano.

Amesema alishawahi kurudishwa nyumbani na mjukuu wake aliyekuwa anaumwa kwa kukosa Sh20,000 ya matibabu.

Furaha ya bibi huyo ilianza kuonekana alipoitwa  jina lake kwa ajili ya kukabidhiwa kadi ya matibabu na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Mariam Msengi, leo Jumatano Septemba 4, 2024.

Mwamvua ni miongoni mwa watu 360 waliopokea kadi za bima ya afya zilizotolewa na shirika lisilo la kiserikali la SOS Children’s Village, kwa watu wenye hali duni wanaoishi katika kata za Kayenze, Sangabuye, Bugogwa na Shibula.

 “Nimefurahi sana kwa sababu wajukuu zangu wanapougua, ukienda kituo cha afya unaandikiwa dawa za kununua lakini unakosa hela ya dawa. Lakini sasa nimefurahi mno,” amesema Mwamvua.

 “Nikaamua kutumia dawa za mitishamba kumtibu homa kali iliyotokana na kuharisha na kutapika, wasamaria wakanipatia hela ya kununua Panadol, nikawa nampa na madawa ya kienyeji namchemshia na kumnywesha, basi Mungu alimsaidia akapona,” amesimulia bibi huyo.

Mwamvua sasa ana uhakika wa matibabu yake na wajukuu zake ambao anawalea baada ya baadhi kufiwa na wazazi na wengine kuachwa nyumbani na binti yake.

Meneja wa SOS Children’s Village Mkoa wa Mwanza, John Masenza amesema bima hiyo ya afya imetolewa kwa kaya masikini ambazo taarifa zao zilitolewa na Serikali za mitaa na kata.

“Tumewezesha kaya 360 kupata kadi za bima kupitia mfuko wa huduma za afya ya jamii iliyoboreshwa kwa sababu afya ni msingi wa kila kitu. SOS inalenga watoto na kuboresha ustawi na malezi yao, hasa wale waliopo kwenye hatari ya kukosa malezi ya wazazi kutokana na hali duni ya kiuchumi,” amesema Masenza.

Mbali na kadi za bima ya afya, vijana 35 walionufaika na mradi wa kuwawezesha kupata ajira wamekabidhiwa pia vifaa vya kazi, zikiwamo mashine za kushona, zana na pembejeo za kilimo na vifaa vya ufundi umeme kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala, Katibu Tawala Msengi amelipongeza shirika hilo na kueleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya afya ili wananchi wapate tiba bora.

Diwani wa Sangabuye, Renatus Mulunga, amesisitiza vijana kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujiongezea kipato.

Related Posts