Dodoma. Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa tuhuma dhidi ya baba anayedaiwa kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa miezi sita.
Limeeleza leo Jumatano Septemba 4, 2024 jalada limepelekwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya hatua zaidi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Jumapili Septemba mosi, katika Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota mkoani Dodoma.
Stephen Damas anadaiwa kumbaka mtoto wake hadi kufa na kisha kuutelekeza mwili nyumbani kwa bibi yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema uchunguzi wa awali kwa kiasi kikubwa umeshakamilika na leo wamewasilisha jalada Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
“Tumewasilisha na wao waweze kuratibu ushahidi ambao umekusanywa na kama kuna maelekezo mengine watupatie, lakini kwa upelelezi wa awali kwa sehemu kubwa tumeshakamilisha ndiyo maana tumewasilisha jalada Ofisi ya Mashtaka,” amesema.
Amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani iwapo ushahidi umejitosheleza na kwamba, wao wanataka kuhakikisha hakuna mianya yoyote ya kisheria ambayo itasababisha kupoteza kesi.
Amesema kwa ushahidi waliokusanya katika kesi hiyo, wana matumaini kuwa haki itapatikana wakati shauri hilo litakapofikishwa mahakamani.
Mama wa mtoto huyo, Stella Gidion jana Septemba 3, akizungumza na Mwananchi alisimulia namna alivyohangaika kumtafuta mwanaye baada ya kuondoka na baba yake.
Akizungumza nyumbani kwake Mbuyuni, Kata ya Kizota, alisema Jumapili Septemba mosi, muwe wake Stephen aliondoka nyumbani na mtoto akiamini amekwenda dukani.
“Nilikaa hadi saa 2.00 usiku nikaona harudi. Nikamwambia mama mwenye nyumba mbona huyu harudi hadi sasa, ngoja nimfuatilie,” alisema.
Alisema alienda dukani hakumkuta, hivyo aliendelea kumtafuta kwenye vilabu viwili vya pombe ambako hakumkuta.
Mama huyo alieleza aliamua kurudia nyumbani ambako aliuliza iwapo amerudi lakini jibu likawa hajarejea.
Alisema alitoka tena kwenda kumtafuta na alipokuwa njiani alimsikia balozi akiongea kwa simu huku akitaja jina lake (mama Eliza) kuwa anamtafuta.
“Nikashtuka kwa nini ananitaja, kuna mtu akamwambia mama Eliza unayemtafuta huyu hapa huku akinieleza kuwa natafutwa na balozi. Nikauliza kwani kuna nini? Nikaambiwa kuna mtoto kaokotwa huko ubalozi wa pili,” alisema.
Alieleza majibu hayo yalimfanya kumweleza naye alikuwa akimtafuta mwanaye aliyeondoka na baba yake. Mama huyo anaeleza walikubaliana waende wote huko alikookotwa mtoto.
Walipofika anasimulia walimkuta mama yake akiwa amempakata mtoto.
“Nikamuuliza nani kamleta huku? Mama akanijibu baba yake. Akasema yeye alikuwa amelala lakini Stephen alimgongea mlango, alipotoka akakuta mtoto amewekwa kwenye kizingiti ndiyo maana ameamua kwenda naye kwa balozi,” alisema.
Alieleza alimhoji iwapo mtoto ni mzima na majibu ya mama yake yalikuwa mwanaye yu mzima.
“Nikamwambia mama naomba nimnyonyeshe, akasema mwache kwanza, utamnyonyesha tu. Tukaenda kituo cha polisi na baadaye tukaja hospitali. Baadaye tuliitwa tena kwenda kutoa maelezo,” alisema.
Alieleza walitoka kituoni akiwa ameongozana na mama yake, balozi na polisi kwenda kumtafuta mtuhumiwa (mume wake) ambaye hawakumpata.
Alisema baada ya kumkosa kwa rafiki na ndugu zake, polisi walimtaka apumzike nyumbani lakini alikataa akitaka kwenda hospitali kumuona mwanaye.
Alisimulia baada ya kung’ang’ania kwenda kumuona mtoto, waliamua kumweleza ukweli kuwa mtoto amefariki dunia hivyo ajikaze na kuvumilia.