Rais Recep Tayyip Erdogan amekutana na Rais Abdel Fattah el-Sisi katika uwanja wa ndege wa Ankara siku ya Jumatano na kisha wote wawili walisafiri ndani ya gari moja hadi ikulu ya rais kwa takriban saa mbili za mazungumzo. Mazungumzo yao yameumulika mzozo unaoendelea huko Ukanda wa Gaza na wote wawili wametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na usambazaji zaidi wa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Palestina waliozingirwa. Rais Erdogan amesema kuwa “Uturuki na Misri zina msimamo wa pamoja kuhusu suala la Palestina. Kukomesha mauaji ya halaiki ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi 11, usitishaji vita wa kudumu haraka iwezekanavyo na usambazaji usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu, ndio vipaumbele vyetu.”Rais El Sissi azuru Uturuki baada ya kumaliza ya muongo mmoja madarakani
Kwa upande wake, Rais Sisi amehimiza juu ya kukomeshwa kwa “mvutano unaozidi kuongezeka katika Ukingo wa Magharibi”, ambako wiki iliyopita wanajeshi wa Israel wamekuwa wakiongoza kampeni ya kijeshi. “Tumeamua kwamba tunapaswa kufanya kazi pamoja ili kuzuia migogoro ya kibinadamu kwa kushughulikia masuala ya kikanda pamoja. Tunapaswa kufanya kazi kwa bidii, hasa kwa ndugu zetu wa Gaza na Palestina,” amesema Al-Sisi.
Uturuki, ambayo imeilaani Israel kwa vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza, imepeleka maelfu ya tani za msaada nchini Misri kwa ajili ya Wapalestina na kusifu juhudi za kibinadamu zinazofanywa na Cairo na jukumu lake katika usuluhishi. Misri, pamoja na Qatar na Marekani, mshirika mkuu wa Israel, imekuwa ikifanya juhudi kwa miezi kadhaa ili kujaribu kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano na kuwarejesha mateka zaidi ya 100 ambao bado wanashikiliwa na kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas.Ni kwa namna gani vita vya Gaza vinawaunganisha Uturuki na Misri?
Kando na hayo, viongozi hao wawili wametia saini jumla ya mikataba 17 ya ushirikiano katika sekta za nishati, hasa gesi asilia na nishati ya nyuklia. Sekta nyingine ni pamoja na ulinzi, utalii, afya, kilimo, fedha, utamaduni, elimu na uchukuzi. Taarifa ya ofisi ya rais wa Uturuki imeongeza kuwa, Erdogan na Al-Sisi walijadili pia uwezekano wa kuiuzia Misri ndege za droni. Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Erdogan ametilia mkazo kuwa Uturuki na Misri zinataka kuimarisha biashara ya kila mwaka kwa dola bilioni 5 hadi kufikia dola bilioni 15 katika miaka mitano ijayo.Uturuki yaiwekea Israel vikwazo vya kibiashara
Suala jingine lililojitokeza wakati wa mazungumzo ni kuhusu Somalia. Hivi karibuni nchi zote mbili zilitia saini mikataba ya ushirikiano wa kijeshi na Somalia, ambayo iko katika mvutano na jimbo lililojitenga la Somaliland baada ya kutia saini makubaliano ya kukodisha eneo la bahari kwa Ethiopia. Kulingana na Rais Sisi viongozi hao pia walijadili hali ya Libya, ambapo nchi hizo mbili zimekuwa zikitofautiana kwa muda mrefu na kuunga mkono pande zinazopingana katika mzozo ambao haujatatuliwa.
Uturuki na Misri zilisitisha uhusiano mnamo mwaka 2013 baada ya Sisi wakati huo akiwa waziri wa ulinzi kumwondoa mamlakani rais Mohamed Morsi aliyekuwa mshirika wa Ankara na sehemu ya vuguvugu la udugu wa Kiislamu.
Mnamo mwezi Februari, Erdogan alizuru Misri kwa mara ya kwanzatangu mwaka 2012 na kueleza juu ya mkakati wa kufufua uhusiano wa nchi hizo mbili. Licha ya miaka kumi ya mfarakano, biashara kati ya nchi hizo mbili haikukoma. Uturuki imekuwa ni mshirika wa tano kwa ukubwa wa kibiashara wa Misri.