Dodoma. Kesi ya kubaka kwa kundi inayomkabili, Fatma Kigondo, afande anayedaiwa kuwatuma vijana kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti Mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam, inakuja mahakamani leo Alhamisi, Septemba 5, 2024 tena.
Kesi hiyo, iliyofunguliwa na Paul Kisabo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, ilishindwa kusikilizwa Agosti 23, 2024 baada ya afande huyo kushindwa kutokea mahakamani.
Uamuzi wa kumpatia hati ya wito kwa mara nyingine, ulitolewa na Hakimu Mkazi wa Dodoma, Fransis Kishenyi anayesikiliza kesi hiyo namba 23627 ya mwaka 2024
Awali, wakili anayemwakilisha Kisabo katika kesi hiyo, Peter Madeleka aliomba Mahakama kutoa utaratibu mwingine wa kumkamata kwa kutoa amri kwa kuwa afande huyo alipata wito wa kuitwa mahakamani Agosti 22, 2024 lakini hakutokea.
“Kwa kuwa ni kosa la jinai na waliokuwa wakitakiwa kutimiza wajibu wao hawakufanya hivyo ndiyo maana na sisi tuko hapa. Tunaomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa,” alidai Madeleka.
Alitaka mahakama kutumia kifungu cha 130 cha mwenendo wa makosa ya jinai kumkamata afande huyo kwa kuwa malalamiko yao yanaangukia katika makosa ya jinai.
Hata hivyo, Hakimu Mkazi Kishenyi alisema kifungu hicho hakilazimishi mahakama kutoa amri ya kukamatwa pekee bali kinatoa fursa pia kutoa hati ya wito.
“Nitatoa hati ya wito nyingine ili nijiridhishe kama hati ya wito tuliyoitoa jana (Agosti 22, 2024) haijamfikia,” amesema.
Afande anadaiwa kutajwa kwenye tukio la vijana wakiwamo askari wawili ambao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kudaiwa kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti wa miaka 17 mkazi ya Yombo mkoani Dar es Salaam.
Tayari washtakiwa wanne wamefunguliwa kesi ya ubakaji kwa kundi na kuingilia kinyume na maumbile binti huyo ambayo iko Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Zabibu Mpangule.
Washtakiwa hao katika kesi namba 23476 ya mwaka 2024 ni Askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, Askari Magereza C1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson, maarufu Machuche na Amin Lema, maarufu Kindamba.