WAZIRI NDEJEMBI AANZA KUSHUGHULIKIA MGOGORO WA NDACHI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi ameagiza kusitishwa kwa shughuli za ujenzi katika eneo la Ndachi jijini Dodoma ambalo limekua likikabiliwa na mgogoro wa muda mrefu.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo jijini tarehe 4 Septemba 2024 Dodoma wakati wa kikao chake cha pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe Rosemary Senyamule, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, Wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi pamoja na wale wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichokua na lengo la kujadili ufumbuzi wa mgogoro huo.

“Ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametutaka kuhakikisha Dodoma haina mgogoro wa ardhi na mfano mzuri uwe katika suala hili la Ndachi kuhakikisha linaisha moja kwa moja. Na katika kulimaliza hili lazima tuunde timu maalum ya kufanya kazi hii” amesema Mhe. Ndejembi.

Mhe. Ndejembi ameelekeza kuwa, ujenzi wowote katika eneo hilo usimame kwa sababu kadri unavyozidi kufanyika bila kibali cha ujenzi ndivyo mgogoro unavyozidi kukua. “Yeyote atakayeanza kujenga kutoka sasa maana yake hataki mgogoro huo utatuliwe na serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa atakayekaidi.” Amesema

Aidha, Mhe. Ndejembi amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga kuunda timu ya wataalamu kutoka wizarani watakaoshirikiana na watalaamu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri ili kufanyia tathmini mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi na ndani ya siku saba timu hiyo iwe imeanza kazi hiyo.

Related Posts