KIUNGO mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho kwa sasa yupo katika kambi ya timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes, huku akifichua kinachoibeba Ligi Kuu Bara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Aucho maarufu kama Dokta, amesema uwekezaji ndiyo sababu kubwa ya Ligi Kuu Bara kuwa na ushawishi kwa nchi nyingine kuifuatilia na kushabikia baadhi ya wachezaji pamoja na timu wanazozichezea.
Kiungo huyo ambaye ni mmoja ya nyota 14 wa Yanga walioitwa katika timu za taifa tofauti kwa mechi za kimataifa za kuwania tiketi ya Afcon 2025, alizitolea mfano Yanga, Simba na Azam FC namna zinavyosajili wachezaji wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wanapocheza ni rahisi kuangaliwa na mashabiki wa nchi walizotokea.
“Nimeona uwekezaji wa soka Tanzania ni mkubwa, ndio maana ligi yao inaonekana ina mvuto wa kuwavuta wachezaji nje ya taifa hilo kuicheza na wamekuwa wanafanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu,” alisema Aucho mwenye umri wa miaka 31 na kuongeza:
“Mfano ni rahisi mashabiki wa Zambia kuwafuatilia kina Clatous Chama, Kennedy Musonda au Joshua Mutale na wengine wanaocheza nje na Yanga, Stephane Aziz Ki watu wa Burkina Faso watamwangalia akicheza, Uganda wataniangalia nikicheza, hivyo lazima ligi hiyo itakuwa na ushawishi mkubwa.”
Aucho alisema uwepo wao kama wageni unasaidia kuibua ushindi dhidi ya wazawa, jambo linalotengeneza na kupatikana kwa wachezaji watakaozisaidia timu zao za taifa.
“Ligi nzuri inatoa wachezaji wazuri, faida ambayo wanaipata wazawa, wanapoonyesha kiwango kizuri, nje na kuzisaidia klabu zao watalifaidisha taifa lao katika mashindano mbalimbali,” alisema Aucho aliyewahi kukipiga Misri, India na mataifa mengine kabla ya kutua Yanga misimu minne iliyopita aliyeongeza:
“Ingawa nimeona mashabiki wengi wanazipenda timu mbili ndizo zilizo na nguvu zaidi ambazo ni Yanga na Simba, pamoja na hilo ligi ipo vizuri.”
Msimu uliopita Aucho hakuwa na bao, alitoa asisti mbili, alicheza mechi 20 dakika 1629, ambapo msimu huu anaamini atafanya makubwa zaidi na yeye na nyota wenzake wa Uganda wapo Afrika Kusini kwa ajili ya mechi itakayopigwa kesho Ijumaa dhidi ya wenyeji Bafana Bafana kabla ya kurudi Kampala kuipokea Congo Brazzaville, Jumatatu ijayo katika mechi za Kundi K kuwania fainali zijazo za Afcon za Morocco.