Tuko tayari kwa mazungumzo na Ukraine – DW – 05.09.2024

Rais Putin amesema makubaliano ya awali yaliyofikiwa mwanzoni mwa vita hivyo baina ya wapatanishi wa Urusi na Ukraine huko Istanbul, ambayo hata hivyo hayakutekelezwa, yanaweza kutumiwa kama msingi wa mazungumzo ya sasa. 

Haya ni miongoni mwa masuala kadhaa aliyoyazungumza Rais Vladimir Putin kwenye kipindi cha maswali na majibu katika Kongamano la Kiuchumi la nchi za Kanda ya Ulaya Mashariki na Asia, linalofanyika mjini Vladivostock.

Amesisitiza kuhusu mazungumzo, lakini yatakayojikita katika makubaliano yaliyotupiliwa mbali kati ya wapatanishi wa Moscow na Kyiv yaliyofikiwa mjini Istanbul, Uturuki mnamo mwaka 2022, ambayo hayakuwekwa hadharani. Ikulu ya Kremlin inasisitiza kwamba mataifa hayo yalikaribia kufikia makubaliano katika majira ya machipuko ya mwaka 2022, muda mfupi baada ya Moscow kuivamia Ukraine.

Kulingana na Putin, makubaliano hayo hayakutekelezwa kwa kuwa Kyiv ilizuiwa na washirika wake Marekani na baadhi ya mataifa ya Ulaya yaliyotaka kufanikisha mkakati wa kuiangusha Urusi.

Soma pia:Putin asema uvamizi wa Ukraine Kursk haujawa na athari

Vita vyaUkraine
Seehemu ya mashambulizi ya Ukraine katika jimbo la Kursk. Urusi inasema mashambulizi hayo yameambulia patupu na hayakuwa na athari yoyotePicha: 95th Air Assault Brigade/via REUTERS

Amezungumzia pia juu ya mashambulizi makubwa ya Ukraine katika jimbo la Kursk, akisema kwa mara nyingine kwamba lengo la uvamizi huo la kuzorotesha mashambulizi ya Urusi hususan katika jimbo la Donbas halikufanikiwa na badala yake Kyiv imelidhoofisha tu jeshi lake na kuliruhusu jeshi la Urusi kuongeza kasi ya mashambulizi, mashariki mwa Ukraine.

“Tunatakiwa kuwafikiria watu wetu ambao wanapitia majaribu na mateso makubwa kutokana na vitendo hivi vya kigaidi. Na wajibu mtakatifu wa Jeshi ni kuhakikisha wanamuondoa adui kwenye maeneo haya pamoja na kuwalinda raia wetu.”  

Idadi ya vifo baada ya shambulizi la Urusi yaongezeka

Anasema hayo wakati taarifa kutoka Kyiv zikisema idadi ya vifo vilivyosababishwa na shambulizi la kombora katika jii la Poltava ikiongezeka na kufikia watu 54 na majeruhi karibu 300. Shambulizi hilo lilifanywa katika Taasisi ya Kijeshi la Poltava, ingawa haiko wazi ikiwa wahanga walikuwa ni wanajeshi ama raia.

Soma pia:Urusi inajitahidi kuwaondoa wanajeshi wa Ukraine Kursk

Watu watano huenda wakawa wamefukiwa chini ya kifusi, kufuatia shambulizi hilo kubwa kabisa miongoni mwa mengineyo kwenye vita hivyo na ambalo limeibua ukosoaji mkali ikiwa ni pamoja na kutoka Washington iliyolilaani vikali na kulielezea kama ukatili mwingine uliofanywa na Putin.

Huku hayo yakiendelea, Rais w Ukraine Volodymyr Zelensky kesho Ijumaa anatarajia kuzuru kambi ya jeshi la anga ya Marekani iliyoko Ujerumani kwa ajili ya mazungumzo kuhusiana na msaada zaidi wa magharibi katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Gazeti la Ujerumani la Spiegel, limeripoti kwamba Zelensky anatarajiwa kutoa wito wa silaha zaidi mpya, ikiwa ni pamoja na makombora ya masafa marefu na mifumo ya kujilinda angani katika kikao cha muungano usio rasmi wa karibu nchi 50 zinazoiunga mkono Ukraine.

Related Posts